Home » » MACHALI, MKURUGENZI WATUNISHIANA MISULI KIKAONI

MACHALI, MKURUGENZI WATUNISHIANA MISULI KIKAONI


Na Mwandishi Wetu, Kasulu

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, William Waziri na Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, walitunishiana misuli kwa kutupiana maneno makali na kunyang’anyana kipaza sauti katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Sakata hilo liliibuka baada ya Machali kuhoji na kutaka ufafanuzi kwa nini hoja yake binafsi aliyoiwasilisha Juni 9, mwaka huu katika ofisi ya Mkurugenzi iwe moja ya ajenda katika kikao hicho na iweze kupatiwa majibu, lakini haikuwepo katika ajenda za kikao hicho.

Wakati akihoji kuhusiana na hoja yake, alisema yote yaliyotokea yanasababishwa na wakuu wa idara na aliwaita wakuu wa idara wa Halmashauri ya Kasulu ni majambazi na wahuni.

“Nasema hivi, siogopi kufa, nimeapa hasa pale ninapotetea maslahi ya wananchi, sababu nimeshaona ujanja ujanja unaofanyika ndani ya halmashauri yetu, sitokubaliana na hali hii hata kidogo,” alisema Machali.

Alisema amechoma mafuta ya gari kutoka bungeni hadi Kasulu kwa ajili ya kuhudhuria kikao hicho kwa kuamini moja ya ajenda itakuwa ni hoja yake binafsi aliyotaka isomwe na kutolewa majibu na yeye awepo katika kikao.

Kwa upande wake, Waziri, alianza kwa kukanusha kauli ya Machali kwamba Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ni majambazi na wahuni kuwa siyo ya kweli.

Hata hivyo, katika hali ambayo haikutegemewa na wajumbe wa kikao hicho, ghafla Machali alisimama tena bila ya ruhusa ya mwenyekiti na kuvuta kipaza sauti toka mkononi kwa mkurugenzi, lakini naye akaking’ang’ania akawa anavuta upande wake, huku baadhi ya madiwani wakipiga kelele za kushangilia.

Baada ya sakata hilo la kugombania kipaza sauti kudumu kwa muda wa takriban dakika nne, ikabidi Mkurugenzi huyo awe mpole na kukaa katika kiti na kumuachia kipaza sauti Machali, aliyekuwa kama mbogo ndani ya kikao.

“Kwa kweli sitokubali kikao kiendelee kwa utaratibu huu hata kidogo, ni bora waheshimiwa madiwani tuahirishe kikao hiki hadi tupange kingine tena, mkurugenzi huna mamlaka hata ya kunitoa nje ya kikao hiki, wewe ni katibu tu kwenye kikao hiki, mwenye mamlaka ya kunitoa humu ni mwenyekiti wa kikao hiki,” alisema Machali.

Naye, Diwani wa Kata ya Nyamidaho, Ignas Bahoga, alisimama na kuanza kumshambulia mkurugenzi kwa kusema yeye kama mtaalamu majibu yake anayoyatoa katika kikao si mazuri.

“Kwa kweli wakuu wa idara wa halmashauri yetu ni jeuri, unapoenda ofisini kwake kupata maelezo ya jambo fulani wanakuzungusha na kukuangalia kama sijui kitu gani, sasa kama kwa sisi waheshimiwa madiwani mnatufanyia hivi je, kwa mwananchi wa kawaida inakuwaje,” alisema Bahoga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kasulu, William Utui, alitumia busara ya kikao kwa kutuliza hali hiyo kwa kusema hoja hiyo binafsi ya Machali italetwa katika kikao kijacho iweze kujadiliwa na kupatiwa majibu.

“Ndugu zangu naona hali ya hewa ya humu ndani imechafuka na tunakoelekea si kuzuri, hapa hatujaja kwa ajili ya kulumbana au kutaka kuonyeshana nani zaidi, tupo hapa kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Kasulu sasa ni vizuri tukafanya yale waliyotutuma hapa,” alisema Utui.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa