Home » » WAKAMATWA KIGOMA WAKIFANYA BIASHARA YA KUSAFIRISHA WATU HAI, KAMA HUKUIPATA NAFASI YA KUISOMA HABARI HII YA KUSISIMUA

WAKAMATWA KIGOMA WAKIFANYA BIASHARA YA KUSAFIRISHA WATU HAI, KAMA HUKUIPATA NAFASI YA KUISOMA HABARI HII YA KUSISIMUA


Kigoma
POLISI mkoani Kigoma inawashikilia watu watatu wakiwemo wafanyakazi wawili wa basi la Osaka linalofanya safari kati ya Kigoma na Dar es Salaam, wakituhumiwa kufanya biashara haramu ya kusafirisha watu hai.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba juzi saa 10 jioni askari wa upelelezi wakiwa katika doria, waliona basi la abiria katika kijiji cha Heru Juu wilayani Kasulu likikusanya watu kwa ajili ya kuwasafirisha.

Alisema katika kufuatilia hayo askari hao wa upelelezi waligundua basi hilo lilifika kijijini hapo kwa ajili ya kuwachukua abiria 44 ambao walikuwa katika mpango wa kuwasafirisha kuwapeleka Msumbiji kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za kukata mbao.

Katika tukio hilo Kamanda huyo wa polisi alisema wanamshikilia mfanyabiashara na mkazi wa jijini Dar es Salaam, Michael Mgala ambaye ndiye aliyekuwa akihusika na kitendo cha kuwakusanya watu hao kwa ajili ya kuwasafirisha.

Alisema jeshi hilo pia linawashikilia watumishi wawili wa basi la Osaka lenye namba za usajili T 481 BFJ, akiwemo dereva Waziri Hadaike na kondakta wake Erick Mangesho. Kwa sasa polisi inaendelea kuwahoji watu hao kubaini kosa lao.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema wamewaachia huru watu hao 44 waliokamatwa katika tukio hilo kwa kile kinachoonekana kwamba hawana kosa katika hilo kwa vile wao ni waathirika.
Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa