Home » » WANAFUNZI WALIOJIUNGA KINYEMELA WAZUILIWA

WANAFUNZI WALIOJIUNGA KINYEMELA WAZUILIWA

Na Rose Mweko, aliyekuwa Kigoma

WANAFUNZI zaidi ya 1,000 katika Shule za Sekondari za Serikali za Mkoa wa Kigoma, wamezuiliwa kuendelea na masomo kutokana na kuingia katika shule hizo kinyemela.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kuwa, wanafunzi hao hawakufaulu darasa la saba lakini wengi wao walisoma katika shule za Serikali kinyemela pasipo kuhakikiwa.

Imebainika kuwa shule za Sekondari za Mwananchi na Nyarubanda zinaongoza kwa kuwa na wanafunzi wa aina hiyo, ambapo wengi wao walifukuzwa baada ya kugunduliwa na wakaguzi.

Wanafunzi hao maarufu kama ‘mamluki’ wamekuwa wakisoma kwa kutumia namba za wanafunzi walioacha shule na wale ambao hawakuripoti kidato cha kwanza na kusajiliwa kwa majina yao bila kuwa na namba za usajili (TSM9).

Mmoja wa walimu katika Shule ya Sekondari Mnanila alikiri kuwapo kwa wanafunzi wa aina hiyo katika shule yake na kueleza kuwa, tatizo hilo ni la muda mrefu.

“Kwa kawaida wanafunzi wanaiongia shule kwa uhalali ni wale waliochaguliwa hivyo TSM9 zao hupelekwa katika shule walizochaguliwa hata kama mwanafunzi atahamishwa shule hupaswa kuhama na TSM9,” alisema.

Wanafunzi wasio halali ni wale walioingia shule kwa njia za mkato, ambapo wengine huingia kwa kutumia nafasi za wanafunzi waliochaguliwa lakini hawakujiunga na shule hizo ama kwa vinginevyo.

Wazazi waliiomba Serikali kuwaonea huruma wanafunzi ambao wamekaribia kuanza mtihani wa kidato cha nne, ili kuwawezesha kufanya mtihani wao kutokana na kuhangaika kwa muda mrefu katika safari yao ya masomo.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa