Home » » WANANCHI WAOMBA UTATUZI WA MGOGORO WA ARDHI

WANANCHI WAOMBA UTATUZI WA MGOGORO WA ARDHI


na Mwemezi Muhingo, Kakonko
WANANCHI wa Kijiji cha Kabare, Kata ya Muhange Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wamemuomba mkuu wa wilaya hiyo, kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo kati yao na viongozi wa kijiji hicho waliompa mwekezaji.
Wakizungumza na Tanzania Daima juzi kijijini hapo, baadhi ya wananchi walimtuhumu Ofisa Mtendaji wa serikali ya kijiji, Laurian Mbasha, kwa kutaka kuwapokonya ardhi yao ili kumpa mwekezaji anayetaka kutumia eneo hilo kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.
Mmoja wa wanakijiji hao, Amos Selubebe alisema kuwa kitendo cha kuchukua eneo ambalo linatumika kwa ajili ya kilimo ni unyanyasaji, pia kinyume na haki za binadamu na sheria za ugawaji ardhi katika vijiji, kwa kuwa eneo hilo ndilo wanalolitegemea kwa shughuli za kilimo na ufugaji.
Selubebe alisema kuwa wao kama wanakijiji hawakuhusishwa hata kidogo ila walikuja kuambiwa tu kwenye mkutano wa hadhara kuwa ardhi iliyoko katika eneo la Lukelela kijijini hapo amepewa mwekezaji hali iliyozua mtafaruku.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa serikali ya kijiji, Mbasha, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema hivi sasa wamesitisha mambo yote baada ya mtafaruku huo kutokea.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakoko, Petro Toyima, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema kuwa hakuwepo kwa muda mrefu, na kwamba atahakikisha ardhi hiyo haiporwi na mwekezaji huyo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa