Home » » ASKARI POLISI WANNE MBARONI KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI

ASKARI POLISI WANNE MBARONI KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI

Na Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu
ASKARI polisi wanne wa kituo cha Polisi Mkugwa kilichopo Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma wanashikiliwa kwa tuhuma za ujambazi baada ya kumpora mwanamke mmoja kiasi cha shilingi milioni mbili na kumjeruhi vibaya kwa mapanga na marungu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Bw. Venance Mwamoto alisema tukio  hilo limetokea usiku wa September 18 mwaka huu katika kijiji cha Kifura, ambapo askari hao walimvamia mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina la  Bi Jenisia Minani mwenye umri wa miaka 36 wakati  alipokuwa akitoka dukani kuelekea nyumbani kwake.
Aidha askari hao ambao hawakutajwa majina yao walifanikiwa kukimbilia katika kituo cha polisi cha Kifura ambapo wananchi wenye hasira kali walikusanyika kwa lengo la kwenda kuwashambulia.
Katika tukio askari ambaye hata hivyo hakufahamika jina lake mara moja alitokeza kuutuliza umati wa wananchi hao lakini jitihada zake zilikoleza moto wa wananchi hao wakidai kutoamini jeshi la polisi na kuomba kuonana na Mkuu wa Wilaya.
Wananchi hao wenye hasira kali walikusanyika na kukivamia kituo cha polisi wakiwa na mapanga na marungu na silaha mbalimbali wakidai kuwa waliofanya kitendo hicho cha kumpora pesa mwanamke huyo na kumjeruhi  ni polisi  hivyo watolewe nje ili wauwe
Mkuu wa wilaya hiyo Bw Mwamoto alilazimika kuwasha gari usiku wa saa nane kuelekea kwenye tukio baada ya kupigiwa simu ili kuwatuliza wananchi hao ambapo aliahidi kulifanyia kazi swala hilo.
Bw Venance Mwamoto ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya kibondo alisema kuwa wanatarajia kuunda tume ndogo kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo.
Bi Jenisia ambaye alijeruhiwa vibaya  katika tukio hilo amelazwa katika hospitali ya wilaya ya kibondo kwa matibabu zaidi.
Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa