Home » » DK. TIZEBA ALIA NA BANDARI YA KIGOMA

DK. TIZEBA ALIA NA BANDARI YA KIGOMA

Na Editha Karlo, Kigoma

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kupeleka wakaguzi wa hesabu katika Bandari ya Kigoma.

Wahasibu hao ni kwa ajili ya kumkagua mwekezaji wa Upakuaji wa Mizigo tawi la Kigoma (MUWAP) na (MSCL), ili kufahamu tija ya utendaji kazi wake na udhibiti wa fedha zinazopatikana.

Tizeba aliyasema hayo jana katika ziara fupi ya kutembelea bandari ya Kigoma yenye lengo la kujua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wafanyakazi wa bandari hiyo.

Waziri huyo aliweza kubaini upungufu katika taarifa alizosomewa na watendaji mbalimbali wa bandari hiyo hususan, kipengele cha mapato na matumizi ya fedha zinazopatikana katika meli.

“Nasema hivi, kabla ya jumamosi ijayo nataka wakaguzi wa hesabu kutoka makao makuu, waje hapa wafanye kazi yao, ili kubaini ukweli wa hizi fedha zinazopatikana katika safari za meli hasa Meli ya Mv Liemba.

“Haiwezekani kabisa mniambie eti meli inafanya safari zake mara mbili kwa mwezi, halafu katika hizo safari mbili moja inakuwa ya hasara nyingine ya faida kwa kweli sikubaliani na hili.

“Kama mnadai safari zenu abiria wanakuwa kwa msimu kwanini kipindi chenye msimu wa abiria wengi ndo msiwe mnasafiri? ili muwe mnapata faida si bure hapo lazima kuna ujanja ujanja tutaujua,” alifoka Tizeba.

Waziri huyo alisema fedha zinaweza kuchukuliwa kirahisi katika bandari hiyo, kutokana na wafanyakazi walio wengi kuwa na mikataba ya muda mfupi, huku wakiwa na dhamana ya kushika fedha za Serikali.

“Haiwezekani mtu anamkataba wa miezi sita ndo anapewa dhamana ya kushika fedha za Serekali, tutamuamini vipi kama siyo wanaishia kuweka kwenye mifuko yao? yeye anakuwa kimaslahi zaidi, mkataba wake ukiisha na yeye anaondoka zake,” alisema.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa