Na Frank Geofray-Jeshi la
Polisi, Kigoma
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma
limeanzisha mfumo wa kuweka kumbukumbu za waendesha bodaboda wote katika wilaya
ya Kigoma ili iwe rahisi kuwapatia mafunzo na kuwasaidia pindi wanapopata
matatizo pamoja na kukabiliana na ajali za barabarani.
Hayo yalisemwa jana na Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi wa Polisi Frasser Kashai wakati wa
hafla fupi ya kuwakabidhi makoti maalumu waendesha bodaboda 350 kutoka vituo 15
vya Wilaya ya Kigoma yatakayowawezesha kutambulika maeneo wanapopaki pikipiki
zao na kuwasaidia pindi wawapo barabarani.
Alisema Mfumo huo maalumu wa kuwatambua
waendesha bodaboda utawasaidia sana abiria na waendesha bodaboda hasa pale
wanapopata matatizo pindi wawapo barabarani kwakuwa itakuwa rahisi kuwatambua.
Kamanda Kashai alisema kuwepo
kwa Mfumo huo kutawasaidia pia abiria kwa kuwa kutawapa fursa kujua
wanapanda pikipiki inayopaki eneo gani hasa kwakuangalia nyuma ya
makoti maalum waliyowapatia.
Aidha katika hatua nyingine
Kamanda Kashai ametoa wito kwa waendesha bodaboda wengine katika Mkoa wa Kigoma
kuiga mfano wa Wilaya ya Kibondo ambayo imefanikiwa sana katika suala la mpanda
pikipiki kuvaa kofia ngumu yeye pamoja na abiria wake.
“Natoa wito kwa wilaya nyingine
za Mkoa wa Kigoma za Kasulu,Uvinza, Kakonko na Buhibwe nao waige mfano wa
waendesha bodaboda wa Kibondo kwakuwa wao wapo mbali sana katika suala hili la
kujilinda na kutambuana hali ambayo inawafanya kuaminiwa na abiria wao” Alisema
Kamanda Kashai
Kwa upande wao waendesha
bodaboda katika wilaya ya Kigoma wamesema wataendelea kuwashauri wenzao
kujiunga katika vikundi ili waweze kutambulika na kupata manufaa ambayo
yatawaweka katika hali ya usalama wao, abiria pamoja na pikipiki zao.
0 comments:
Post a Comment