Home » » Madiwani Kasulu watakiwa kujaza fomu za NHIF

Madiwani Kasulu watakiwa kujaza fomu za NHIF

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, wamehamasishwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani hapa kujaza fomu ili waweze kupatiwa vitambulisho vyao kwa ajili ya matibabu. Meneja wa Mfuko wa Bima ya afya Mkoa wa Kigoma, Elius Odhiambo, alitoa wito huo kwa madiwani hao mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani humo.
Odhiambo, alisema madiwani wameingizwa kwenye mfuko huo kwa mujibu wa sheria namba 3 ya mwaka 2009, ambapo wengi wao hudhani kuwa wakianza kukatwa fedha za matibabu moja kwa moja hupatiwa matibabu bila kujaza fomu maalumu kwa ajili ya kitambulisho.

“Ninachowaomba madiwani ambao hadi sasa bado hamjajaza fomu, sasa jazeni haraka ili muweze kupata vitambulisho vyenu vya matibabu unapokuja hauna taarifa sasa hutoweza kupatiwa matibabu.

“Ni wazi kila mtu ni mgonjwa mtarajiwa, lakini kupitia mfumo huu wa NHIF ni wazi ndugu zangu mtakuwa na uhakika wa matibabu ambapo hadi sasa kati ya madiniwa 56, ni madiwani saba tu ndio waliojaza fomu,” alisema Odhiambo.

Meneja huyo alisema anasikitika kwa kitendo cha madiwani kuchelewa kujaza fomu za taarifa zao na wategemezi wao kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya matibabu pindi watakapougua au kuuguliwa na wategemezi wao.

Sambamba na hilo, Odhiambo aliipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kwa kuwasilisha malipo yao kwa muda muafaka.

Chanzo Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa