Home » » `Chadema haijakurupuka kuwasimamisha Zitto, Kitila`

`Chadema haijakurupuka kuwasimamisha Zitto, Kitila`

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameanza ziara katika Jimbo la Kigoma Kaskazini linalowakilishwa na  Zitto Kabwe, huku akiwaeleza wananchi kuwa chama hicho hakikirupuka kumsimamisha uongozi Zitto kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Aidha, amewalipua wenyeviti wa Chadema waliojizulu baada ya sakata la Zitto kwa kusema kuwa wamefanya hivyo kutokana na kupewa fedha ambazo mmoja wao zimemsaidia kujenga nyumba haraka.

Wenyeviti wa Chadema waliojiuzulu ni Wilfred Kitandu wa mkoa wa Singida na Ally Chitanda wa Lindi, ambao walifikia uamuzi huo baada ya Zitto kuvuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, ambaye alivuliwa ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Hata hivyo, Dk. Slaa hakufafanua kama wenyeviti hao walihogwa na nani.

Akizungumza jana na mamia ya wananchi wa kijiji cha Nyalubanda Jimbo la Kigoma Kaskazini waliohoji sababu za Chadema kuchukua hatua za kumsimamisha Zitto uongozi, alisema chama hicho kinafanya kazi kwa kuzingatia katiba yake.

Dk. Slaa akihutubia wananchi hao huku mvua ikinyesha iliyoambatana na ukungu mzito, alisema katiba ya Chadema haina kipengele kinachotaka chama hicho kinapotaka kuchukua hatua dhidi ya kiongozi au mwanachama aliyefanya kosa hadi suala hilo waulizwe wananchi.

"Nilichogundua wenyeviti waliojiuzulu nyadhifa zao wamenunuliwa kwa pesa na mmoja wao baada ya siku mbili tatu, alijenga nyumba na amekuja kupiga magoti akiomba arudi Chadema, lakini hatuwezi kumkubalia," alisema Dk. Slaa bila kumtaja jina.

Dk. Slaa alisema wananchi na wanachama lazima watambue kuwa Chadema haijawahi kutetereka toka mwaka 2011, hivyo wanaodhani inaweza kutokea hivyo baada ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya Zitto wanajidanganya.

Alisema kiongozi yeyote au mwanachama atakayekiuka au kuvunja maadili na misingi ya katiba ya chama hicho awe ni Dk. Slaa, Mbowe au Mtei, lazima atachukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na katiba.

Alitoa mfano mwaka 2011 madiwani wa Chadema mkoa wa Arusha walipobainika kukiuka kanuni za chama, walichukuliwa hatua na hadi sasa chama hakijayumba na kinadunda.

Alisema wananchi wakiwamo wa Kigoma wasiumize kichwa kwa hatua zilizokwisha chukuliwa dhidi ya Zitto kwa sababu suala hilo siyo la kwanza kuchukuliwa kwa kiongozi anayebainika kukiuka katiba ya chama.

Dk. Slaa alisema kabla ya Zitto, Dk. Kitila na Samson Mwigamba, kuchukuliwa hatua hizo, waliitwa na kuhojiwa kwenye vikao vya chama.

"Utakuwa mtu wa ajabu una kansa inakutafuna unataka uiache iendelee kukutafuna hadi kwenye moyo ambako huwezi kukata ni bora kuikata kabla haijafika sehemu ambayo haitawezekana kukatwa," alisema.

Dk. Slaa alisema hatua zilizochukuliwa dhidi ya Zitto hazina uhusiano wowote na suala la Zitto kuhoji ukaguzi wa hesabu katika vyama.

Juzi, Dk. Slaa alipowasili mjini Kigoma alipokelewa kwa kishindo na mamia ya wananchi huku pikipiki zaidi ya 150 na magari zaidi ya 20 yakiandamana kumlaki.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa