Home » » Zitto akata rufani Chadema

Zitto akata rufani Chadema

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, amewasilisha nia yake ya kukata rufani kupinga hatua iliyochukuliwa dhidi yake ya kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya chama hicho. Pamoja na kukata rufani hiyo, Zitto pia amewasilisha kimaandishi utetezi wake dhidi ya makosa 11 aliyoshitakiwa nayo, baada ya kuvuliwa nyadhifa, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.
Wakati akichukua hatua hizo, Zitto amewataka wanachama wa Chadema kuwa watulivu kusubiri hatua itakayofuata.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Zitto, Wakili wake, Albert Msando alisema, Zitto ameamua kukata rufani akidai utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu walizochukuliwa yeye, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, ulikiukwa lakini pia sababu za kuchukuliwa hatua hizo hazikuwa sahihi.

Alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za uendeshaji wa chama, utaratibu unaotakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi ambapo kanuni ya uendeshaji namba 6.5.6 inayosema kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu mashitaka kwa maandishi.

“Pia kanuni ya uendeshaji 6.5.2 (a), (b), (c) na (d) kama ilivyorekebiswa Januari, mwaka 2013 inasema, kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya katiba, mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kwanza kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika.

“Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa, Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu (b), (c) hapo juu kama itaona maslahi ya chama kwa ujumla yanaweza kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika,” alisema Msando akinukuu baadhi ya vipengele vya katiba ya chama hicho.

Msando alisema kutokana na hatua hiyo, uongozi wa chama hicho ulifanya mkutano na waandishi wa habari Novemba 26, mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ulisema kwamba marekebisho hayo ya kanuni ya mwaka 2013 ambayo ndiyo utaratibu waliofuata.

“Mabadiliko haya ambayo ni katika kipengele (d), kuhusu hatua ya dharura iliyochukuliwa na Kamati Kuu haikugusa kipengele (a) cha Kanuni.

“Yaani ni kuwa hata kama Kamati Kuu itachukua hatua ya dharura kwa mujibu wa kipengele (d), bado kipengele (a) ni lazima kifuatwe na inatamka wazi sharti la kiongozi kupewa mashitaka kwa maandishi na kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi, hii ni haki ya msingi kwa kila utawala au uongozi.

“Zitto, hakupewa mashitaka yake aliyakuta ndani ya kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au sms).

“Kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa uongozi na kwa kuangalia athari zake kwake yeye binafsi na chama kwa ujumla, Kamati Kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba kanuni za uendeshaji na katiba zinafuatwa,” alisema Msando.

Msando alisema, hatua hiyo inaendana na utaratibu uliotumika kwa Mwigamba, kuvuliwa wadhifa wake wa uenyekiti wa mkoa.

Alisema Mwigamba pia hakuitwa kabisa kwenye kikao hicho na kwamba huo ni ukiukwaji wa kanuni ya uendeshaji inayotamka kwamba lazima kiongozi huyo aitwe kwenye kikao.

Kwa mujibu wa Msando, sababu zilizotumika kwa Zitto, ingawa hajapokea taarifa rasmi ya maandishi kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji, ni kwamba yeye ameshiriki kwenye kuandaa na kusambaza waraka ambao unasemekana ni mkakati wa ushindi wenye lengo la kupindua uongozi uliopo.

“Waraka huo haukumtaja Zitto Zuberi kama muandaaji au msambazaji, waliouandaa hawajaukana na badala yake wamesema wazi wazi kabisa kwa maneno na maandishi kwamba, Zitto hahusiki.

“Si sawa kumuadhibu Zitto kwa hisia au tu kwa sababu ya urafiki wake na watu fulani, haya ni mapungufu ambayo kwa bahati nzuri katiba na kanuni za uendeshaji zinatoa nafasi ya kurekebishwa kwa kutoa nafasi ya kukata rufaa.

“Ibara ya 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama inasema, kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho na rufaa hiyo ifanyike ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu,” alisema.

Alisema kanuni za uendeshaji zinatoa utaratibu unaotakiwa kufuatwa ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia haki yake ya kukata rufani.

Msando alisema kanuni ya 6.5.8 ya kanuni za uendeshaji inasema kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi ya maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani.

Alifafanua kanuni ya 6.5.9 ya kanuni za uendeshaji, mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabu.

“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu.

“Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku 14 baada ya kikao cha maamuzi, lakini hadi hivi sasa hatujapokea taarifa kamili ya mwenendo wa shauri tangu kikao cha Kamati Kuu cha Novemba 20.

“Huo ndio utaratibu ambao Zitto ameamua kufuata kwa kuheshimu maamuzi ya Kamati Kuu lakini kukatia rufaa maamuzi hayo, kuheshimu maamuzi si kukubali uhalali wake,” alisema Msando.

Katika hatua nyingine, Msando alisema kumekuwa na matukio ya kusikitisha ambayo mengine yamefikia mahali kuwa fujo na vurugu ikiwa ni pamoja na kurushiwa mawe Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbrod Slaa.

Alisema vurugu hizo baadhi zimehusishwa na Zitto na baadhi ya watu kwamba anawalipa wenyeviti wa mikoa kutoa matamko ya kujiuzulu, waandishi wa habari ili wasiripoti vizuri mikutano yake, watu kuandamana na kufanya vurugu, ambapo alisema Zitto hahusiki kwa njia yoyote.

Katika hatua nyingine, Esther Mbussi anaripoti kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amewasilisha malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kumuomba atoe mwongozo kuhusu mgogoro uliopo ndani ya chama hicho.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mwigamba kujitokeza na kuzungumza mbele ya waandishi wa habari tangu kuvuliwa wadhifa wake wa uenyekiti wa Chadema Novemba 22, mwaka huu.

Alisema katika malalamiko yake hayo, anamuomba Msajili kuingilia kati na kutoa mwongozo kuhusu mgogoro wa kikatiba ndani ya chama hicho hususani katika kipengele cha katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume cha utaratibu.

“Katiba ya Chadema ya mwaka 2004, kipengele 6.3.2 (c) kinasema, kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi, ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.

“Hata hivyo katiba ya chama ya mwaka 2006 kipengele cha 6.3.2 ( c) inayozungumzia muda wa uongozi inasema, Kiongozi aliyemaliza muda wa ungozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi,” alisema.

Mwigamba alisema sentensi kuhusu ukomo wa uongozi haipo, ingawa ni kweli kwamba marekebisho ya katiba yalifanyika mwaka 2006 ambapo baadhi ya vifungu viling’olewa wakati wa uhariri bila wao kujua.

Alisema hoja ya kubadili kipengele hicho haikuwepo na muhtasari zinaonyesha wazi kuwa kulikuwa hakuna mjadala wa kipengele hicho au kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa si kweli kwamba Chadema haijawahi kuwa na katiba ambayo ina ukomo wa uongozi.

“Pia si kweli kwamba mwaka 2006 katiba mpya iliandikwa upya bali marekebisho yalifanywa kwa baadhi ya vipengele, ila kipengele 5.3.2 (c ) hakikujadiliwa.

“Natumaini kuwa Msajili wa vyama ataweza kutupatia hekima zake na kutoa mwongozo ili suala hili lipatiwe suluhisho la kudumu ndani ya chama chetu,” alisema Mwigamba.

Chanzo;mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa