Home » » Chadema kuwahoji Zitto, Kitila, Mwigamba Ijumaa

Chadema kuwahoji Zitto, Kitila, Mwigamba Ijumaa

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
 
Hatima ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na wenzake waliovuliwa nyadhifa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), itajulikana Ijumaa wiki hii wakati Kamati Kuu ya chama hicho itakapokutana kuzungumzia sakata hilo na kutoa maamuzi ya mwisho.
Afisa Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa chama kimewaandikia barua ya kuitwa mbele ya kikao ili wasikilizwe.

Mbali na Zitto aliyevuliwa unaibu katibu mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, wengine waliovuliwa nafasi zao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, Novemba 22, mwaka huu kwa tuhuma za kukisaliti chama.

“Chama kimewaandikia barua hiyo baada ya kuwa kimeshawaandikia barua ya kuwajulisha kuwa kimeshapokea maelezo yao ya maandishi kuhusu tuhuma 11 walizotuhumiwa nazo. Kwa hiyo wametakiwa kufika kwenye kikao cha Kamati Kuu Januari 3, mwakani (Ijumaa) ,” alisema.

Makene alisema wameitwa ili wasikilizwe kutoka midomoni mwao kuhusu tuhuma zinazowakabili na kwamba hilo limefanyika kwa mujibu wa kanuni ya uendeshaji chama, katika kifungu cha 6.5.2 (b) na 6.5.2 (d).

Alisema kifungu hicho kinaelekeza kwamba Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu wa (b) na (c) kama itaona maslahi ya chama kwa ujumla yako hatarini.

“Lakini katika kuchukua hatua hizo za dharura, mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika. Hivyo chama baada ya kupokea maelezo yao ya maandishi sasa wameitwa wajieleze kwa mdomo. Kila kitu kinakwenda kwa utaratibu hapa,” alisema.

Makene alisema tangu mwanzo chama kiliweka utaratibu kwa kuzingatia katiba, kanuni, maadili, taratibu na miongozo ya chama, ndiyo maana ya taasisi. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa