Kigoma. Wakazi wa Mkoa wa Kigoma, wametakiwa
kujikita katika ufugaji wa samaki kwa kuzingatia kuwa mkoa huo una maji
na ardhi ya kutosha kufanya shughuli hizo.
Wito huo ulitolewa juzi na Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila, alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu
mikakati ya kuondoa umaskini katika jamii.
Alisema ingawa Mkoa wa Kigoma una mabwawa katika sehemu mbalimbali, lakini ufugaji wa samaki bado ni wa kiwango cha chini.
“Haiwezekani wananchi waliopo kwenye fursa kama
hii ya kwetu (Kigoma) washindwe kufuga samaki kikamilifu na badala yake
wanategemea zaidi samaki kutoka Ziwa Tanganyika ambako uvuvi unaofanyika
ni wa kizamani sana,” alisema Kafulila.
Aliwataka maofisa kilimo na mifugo kuwa chachu
kwa kuwaelimisha wananchi juu ya ufugaji wa samaki utakaosaidia kuinua
vipato vyao.
Kafulila pia alishauri halmashauri za wilaya na
manispaa mkoani Kigoma, kufikiria namna ya kuwajengea uwezo watu ili
hatimaye, wamudu kuanzisha miradi ya kufuga samaki.
Kuhusu ufugaji wa ng’ombe mkoani humo, alisema
bado ni wa kiwango cha chini. “Ufugaji wa ng’ombe ni rasilimali muhimu
katika jamii na maeneo ambayo Serikali Kuu na halmashauri zimeweka
utaratibu mzuri zimejikuta zikipata mafanikio makubwa ya kiuchumi na
kijamii,” alisema Kafulila.
Aliisihi Serikali kuweka mifumo thabiti ya
kuwakomboa wafugaji ili waweze kufuga kitaalamu na kwa kiwango bora
kinachokubalika na hatimaye kuwawezesha kupata fedha.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment