“Naomba nichukue nafasi hii kumwomba Rais Kikwete amwondoe Pinda katika 
nafasi hiyo, la sivyo akimwacha ajue Serikali itakuwa legelege, 
haitaweza kutekeleza wajibu wake ipasavyo.”
David Kafulila.
Kafulila amesema udhaifu huo unatokana na baadhi 
ya watendaji wa Serikali kumdharau Pinda kwa sababu kiongozi huyo siyo 
mkali kwa watu wanaokwenda kinyume na maadili, miko ya uongozi, pamoja 
na wale wanaofanya uzembe kazini na kujihusisha na ufisadi.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo kwenye mikutano ya 
hadhara katika Vijiji vya Uvinza, Kandaga na Nguruka alipokwenda kueleza
 mafanikio na changamoto alizopata katika miaka mitatu ya uongozi wake.
Kauli hiyo inakuja ikiwa zimepita wiki mbili tangu
 Waziri Pinda alipolieleza gazeti kwamba atazungumzia shinikizo la 
kutakiwa kujiuzulu linalotolewa na wabunge mbalimbali, baada ya Sikukuu 
ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Shinikizo la kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu liliibuka
 upya baada ya kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa utekelezaji wa 
Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilisababisha Rais Jakaya Kikwete 
kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne, huku baadhi ya wabunge wakimtaka
 Pinda naye aachie ngazi.
Jana Mwandishi wa Habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu, 
Irene Bwire alipoulizwa juu ya suala hilo alisema, “Mheshimiwa Pinda 
hakuwepo na amerudi jana tu (juzi), ila si aliwaahidi kuwa atazungumza 
baada ya sikukuu, subirini atazungumza tu.”
Katika mkutano wake wa hadhara Kafulila alisema, 
“Waziri Mkuu Pinda hatoshi na amepwaya, baadhi ya mawaziri wanamdharau 
na ndiyo maana wengi hupuuza hata kuhudhuria vikao vya Bunge. Kwa hali 
ilivyo sasa nchi hii inahitaji Waziri Mkuu ambaye kama mawaziri 
hawamheshimu, ni lazima wamuogope,” alisema Kafulila.
Alisema Waziri Mkuu amekuwa na lugha laini na 
isiyotisha kwa watendaji wa chini yake kiasi kwamba hakuna anayehofu 
hata inapotokea waziri huyo anafanya ziara mikoani kama ilivyowahi 
kutokea kwa baadhi ya wawaziri waliotangulia kabla yake.
“Mara nyingi utamsikia Waziri Mkuu akijibu maswali
 ya Wabunge kwamba; tutaangalia, bado tunatafakari, mara oooh tuvute 
subira kidogo, tutachukua hatua. Majibu ya namna hii kwa kiongozi mkuu 
wa Serikali ni hatari na yameendelea kuwapa kiburi wasaidizi wake kiasi 
kwamba hawahofu tena kuchukuliwa hatua za kinidhamu, hizi kauli 
zinaathiri ustawi na maendeleo ya wananchi” alifafanua Kafulila.
Amesema njia pekee ya kuleta nidhamu ni kuondolewa
 kwa Pinda Serikalini na kuteuliwa mtu mwingine atakayesimamia kwa dhati
 majukumu ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti rushwa ambayo 
imekithiri zaidi katika Serikali za Mitaa.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment