Serikali wilayani Kakonko mkoani Kigoma, imelipiga marufuku kanisa moja la dini ya Kikristo linaloitwa Sabato Matengenezo, ambalo limeanzishwa na watu sita ambao kwa sasa wanashikiliwa polisi.
Waumini hao wanadaiwa kuwanyima haki za msingi
watoto wao, ikiwamo kuwakataza kwenda shule, kupata matibabu katika
hospitali na zahanati kwa kile wanachodai kuwa imani ya dini yao
hairuhusu.
Habari kutoka kijijini hapo, zinasema kutokana na
tukio hilo, watoto wawili wamefariki dunia baada ya wazazi wao kuacha
kuwapeleka hospitali kwa kile walichodai kuwa ni kimyume na imani ya
dini yao.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kigoma, Dismas
Kisufi alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo pamoja na vifo hivyo alisema
hajapata taarifa ya tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Peter Toyima naye
alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kuwa na taarifa kuhusu
kanisa hilo na kusema kanisa hilo jipya limekuja na sera ya kuwazuia
watoto wao kwenda shule, hospitali kupata matibabu na kulipa nauli
wanapokuwa katika vyombo vya usafiri, hatua inayopingana na azma ya
Serikali kutaka watoto wapate haki zao za msingi. “Serikali haitakuwa
tayari kuona baadhi ya watu wanazuia haki za msingi za watoto wao kwa
kuwakataza kwenda shule, kupata matibabu katika hospitali au zahanati
kwa kisingizio cha imani za kidini, jambo hili haliwezi kukubalika,”
alisema Toyima.
Waumini hao wanaoshikiliwa na polisi katika Kituo
Kikuu cha Polisi Kakonko wametajwa kuwa ni; Ndayizeye Gervas, Majaliwa
Gervas, Paschal Silvanus, Inocent Ernest, Medadi Laurent na Julietha
Medadi ambao ni wakazi wa Kijiji cha Nyabibuye, Kata ya Rumashi wilayani
Kakonko na wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka wananchi kuachana
na dini zisizoeleweka na zinazoleta mifarakano katika jamii, na wakati
wengine wakisisitiza kuwapatia elimu watoto wao, kanisa hilo linakataza
kusomesha watoto kwa madai kwamba kuwapeleka shule na hospitali ni
dhambi kwa Mungu.
Alisema jitihada za Serikali wilayani Kakonko
zimesaidia kuwachukua watoto wawili waliofaulu kwenda Sekondari za
Kanyonza na Nyamtukuza na kuwawezesha kuanza masomo ya kidato cha
kwanza.
Kanisa hilo jipya linadaiwa kujimega kutoka katika
Kanisa la Sabato ambalo ni mojawapo ya makanisa yenye idadi ndogo ya
waumini mkoani Kigoma ikilinganishwa na Kanisa Katoliki, Anglikana na
Assemblies of God.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment