Kumefanyika harakati nyingi za kukomesha vitendo hivi, hata hivyo bado vinaendelea.
Ilikuwa ni saa moja na nusu jioni siku ya
jumapili wakati, Anaheri (siyo jina lake halisi) alipokuwa akitoka
dukani alikotumwa na mama yake. Si yeye wala mama yake waliokuwa na
wasiwasi wowote, kwani mara kadhaa amekuwa akitumwa nyakati hizo.
Lakini kama balaa linavyoweza kushtukiza, siku
hiyo Anaheri, alikamatwa na wanaume wawili waliokuwa wamejificha
kichakani. Wakamziba mdomo na kumwingilia. Hawakuishia hapo, waliamua
kumvunja shingo na kumuua binti huyo mwenye miaka 11 tu.
Hii ndiyo hali halisi nchini, ubakaji na ulawiti vimeshika kasi kiasi cha kutishia amani, utulivu na uhuru.
Takwimu za Kitaifa za makosa ya unyanyasaji wa
kijinsia kwa mwaka 2012 zinaonyesha wanawake 5745 walibakwa kwa mwaka.
Kati yao wanawake wenye umri wa miaka 19 na kuendelea walikuwa 5389 na
watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 walikuwa 356.
Makosa hayo hayakuishia hapo kwani wanaume na
wanawake pia waliendelea kulawitiwa, kwa mwaka 2012 pekee wanaume 691
walilawitiwa. Kati yao, wanaume waliolawitiwa wenye umri wa zaidi ya
miaka 18 ni 456 na watoto ni 235.
Wanawake pia hawakuachwa kwani kwa mwaka huo
huo, wanawake 35 walilawitiwa ambao walikuwa na umri wa miaka 19 na
kuendelea wakati watoto waliolawitiwa walikuwa ni 11.
Vilevile mauaji ya vikongwe yaliendelea kwa kasi
kubwa, kwa mwaka 2012, vikongwe 629 waliuawa. Kati ya hao, wanawake
walikuwa 402 na wanaume 227.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jnsia na Watoto,
Sophia Simba anasema kazi kubwa ambayo wizara ilifanya ni kuunda sheria
kali kuwaadhibu wabakaji na walawiti.
“Kwa jambo hili la kuunda sheria nafikiri
tumefanikiwa kwa sababu adhabu ya miaka 30 si ndogo, lakini tunahitaji
wanajamii washiriki kuzuia ubakaji,” anasema.
Waziri Simba pia anawataka waandishi wa habari
kufanya kazi ya ziada ili kuripoti kuhusu ubakaji kwa kuandika, kufanya
utafiti na kuhamasisha.
Naibu Kamishna Mkuu wa Polisi, Adolphina Chialo
anasema unyanyasaji bado ni tishio kwa Watanzania licha ya juhudi
kufanyika kila siku kuwachukulia hatua wanaofanya uhalifu huo.
Chialo anasema matukio ambayo huripotiwa ndiyo yaliyowekwa kwenye takwimu, hivyo kuna uwezekano kuwa yapo matukio ambayo hayaripotiwi.
Chialo anasema matukio ambayo huripotiwa ndiyo yaliyowekwa kwenye takwimu, hivyo kuna uwezekano kuwa yapo matukio ambayo hayaripotiwi.
“Zamani kesi kama hizi zilikuwa zinaripotiwa
chumba cha mashtaka polisi, lakini tuliamua kuanzisha Dawati la Jinsia
kwa ajili ya usiri wake. Dawati hili linapokea malalamiko kutoka kwa
wanaume, wanawake na watoto. Tunaposema jinsia hatumaanishi ni wanawake
pekee,” anasema
Anasema unyanyasaji wa aina zote upo na kuongeza
kuwa hapo zamani wanawake pekee ndiyo walioonekana kunyanyasika lakini
hivi sasa, hata wanaume wananyanyasika.
Kwa mfano, wapo wanaume ambao wananyanyaswa na
wake zao lakini si kwa kupigwa au kubakwa bali matusi na kunyimwa baadhi
ya huduma hasa kipato kinaposhuka.
“Wanaume wanafika hapa, wanaeleza manyanyaso yao
wanayoyapata kutoka kwa wake zao na hatua zinachukuliwa. Kwa mfano
mawasiliano, kupikiwa, ” anasema.
Anasema suala kubwa zaidi ni ubakaji na vipigo ambapo vipigo vinahusisha watoto kuchomwa moto na kutukanwa.
“Sasa hivi haya matukio yanaonekana kuwa mengi kwa
sababu yanaripotiwa. Zamani watu walikuwa wanayaficha au wanadhani
hakuna pa kuripoti lakini sasa hivi wamejua kuwa kuna suluhisho,”
anasema.
Anasema mikoa ambayo ilidhaniwa kuwa ingekuwa na
matukio mengi ya ubakaji, kama Mwanza na Kagera haina matukio mengi kwa
sababu ya mila zinazowazunguka.
Kwa mfano, Wilaya ya Kinondoni, mikoa ya Mbeya na
Morogoro ilikuwa na matukio mengi zaidi ya ubakaji kuliko Kagera,
Mwanza au Tarime jambo ambalo Kamishna Chialo anasema linasababishwa na
mila. Kinondoni ina matukio 414 ya ubakaji.
“Kwa mfano Mwanza, kuna hii mila ya Chagulaga,
kwao mwanamke hawezi kuripoti kwa sababu kwao ni sehemu ya mila. Lakini
kwa sababu ya elimu baadhi ya mikoa imeamka na wanaripoti,” anasema.
Anasema unyanyasaji wa kipigo na mashambulizi pia
hauripotiwi kwenye baadhi ya maeneo kwa sababu ya mila. Kwa baadhi ya
mila ni haki na sheria kwa mwanamke kupigwa na mume wake.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment