MBUNGE wa Kasulu Mjini
mkoani Kigoma, Bw. Moses Machali (NCCR-Mageuzi), juzi amejikuta
akizomewa baada ya kutoa kauli za kuwaponda baadhi ya viongozi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Bw. Machali alipatwa na
kadhia hiyo katika stendi ya zamani iliyopo Mjini Nansio, Wilaya ya
Ukerewe, mkoani Mwanza wakati akihutubia mkutano wa hadhara.
Akiwa
jukwaani, Bw. Machali alijikuta akizomewa kila alipotoa kauli za
kuelezea maovu ya viongozi wa CHADEMA hasa alipozielekeza kwa Mwenyekiti
wake, Freeman Mbowe.
Katika mkutano huo, mbunge huyo alisema hakuna
watu wabaya kama viongozi wa CHADEMA hasa Bw. Mbowe ambaye pia ni
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni.
Alisema Bw. Mbowe aliwahi
kusimama bungeni na kutaka matumizi mabaya ya fedha za Serikali na
ununuzi wa magari ya kifahari yakome lakini baada ya kurudisha gari
alilopewa na Serikali alilifuata na kuendelea kulitumia.
Kauli hiyo
na nyingine za kuwatuhumu baadhi ya wabunge wa CHADEMA kushiriki katika
ufisadi hasa wa kupokea posho za kwenda nje ya nchi, zilisababisha Bw.
Machali azomewe baadhi ya watu wakimtaka afunge mkutano na kuondoka.
Kelele
za kushinikiza aondoke zilimfanya akatishe hotuba yake mara kwa mara
baadhi ya watu wakidai alitumwa na wabaya wa CHADEMA ili kuwaponda
viongozi wao.
Kutokana na shinikizo hilo, Bw. Machali alisema
ataendelea kuzungumza ukweli kuhusu kiongozi na mtu yeyote mwenye
mienendo isiyofaa bila kujali ni kiongozi kutoka chama gani.
Hata
hivyo, utulivu ilirejea aliposema 'People' na wananchi kumjibu 'Power',
ndipo akaendelea na mkutano wake akiituhumu Serikali kwa kushindwa
kuboresha maisha ya Watanzania badala yake inawabebesha mzigo mkubwa wa
kodi.
Alionya kuwa, Taifa haliwezi kupata maendeleo kama Serikali
itaendelea kuingia mikataba mibovu ya uchimbaji madini na kuwanufaisha
watu wachache.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment