Ujenzi wa Soko la Kimataifa katika Kijiji cha Kagunga,
Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani hapa jirani na mpaka wa Tanzania
na Burundi linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha kibiashara katika
nchi za maziwa makuu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,
Miriam Mmbaga amesema, ujenzi huo wa soko unatarajiwa kutumia Sh2
bilioni hadi kukamilika na litaongeza fursa za kiuchumi na kuchochea
ukuaji wa ajira kwa wananchi wa nchi hizo tatu za Ukanda wa Maziwa
Makuu.
Alisema bidhaa za uvuvi na kilimo ambazo
zinazalishwa kwa wingi na wananchi katika maeneo hayo, zinatajwa
kuwanufaisha wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana soko la
uhakika la kuuza bidhaa zao, badala yake huzisafirisha Burundi ambako
soko lake halina uhakika.
“Licha ya biashara hizo za mazao ya kilimo na
uvuvi, pia tunatarajia bidhaa nyingine za viwandani zitauzwa sokoni
hapo, na jambo hilo litainua uchumi wetu kama halmashauri na taifa,
kutokana na wananchi wetu kujipatia kipato sanjali na kukusanya ushuru
na kodi za Serikali,” alisema Mmbaga.
Mkurugenzi huo ametaja changamoto ya ukosefu wa
barabara inayokwenda kijijini hapo kama kikwazo kikubwa kinachokwamisha
harakati za wafanya biashara kuwekeza kwa kasi katika soko hilo la aina
yake mkoani hapa.
“Hakuna barabara inayounganisha Mji wa Kigoma na
Kijiji hicho cha Kagunga,hii inafanya usafiri pekee unaotegemewa kuwa
kwa njia ya boti katika Ziwa Tanganyika, ambapo mara kadhaa hutokea
ajali ya kuzama, kitendo kinachofanya mali kupotea ziwani na nyingine
kuharibika. Hii ni changamoto kubwa kwetu,” alisema Mmbaga.
Pia ufinyu wa bajeti inayopelekea ucheleweshaji wa
mradi huo, ingawa kwa sasa wamepata mbia ambaye ni Benki ya Rasilimali
Tanzania (TIB) ambao wanatarajia kutoa fedha za ujenzi huo zinazofikia
Sh2 bilioni kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi.
Ujenzi wa soko hilo ulioanza mwaka 2009 tayari
umetumia Sh365 milioni kutoka mapato ya ndani ya halmashauri na kuna
mkakati wa kutenga Sh500 milioni.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment