Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Watu wengi wanasema mzazi mwenye busara siku zote hujitahidi kuweka akiba kwa matumizi ya familia yake.
Akiba hiyo ndiyo huwa mkombozi kwa familia ile hasa wakati wa shida au hali ya hewa inapobadilika na mavuno kuwa haba.
Hata hivyo, kwa mtu ambaye ni mtumishi iwe 
serikalini au kokote kwingine katika Tanzania ni vigumu kwake kuweka 
akiba hasa kwa fedha inayopatikana kwenye mshahara na marupurupu 
mengine.
Swali la msingi ni kuwa je, anawezaje mtumishi wa 
serikali kuishi vizuri nchini Tanzania wakati ana kipato ambacho 
hakilingani au hakiendani na hali halisi ya maisha?
Pengine jiulize, anaishi vipi Mtanzania ambaye 
anachuma kiasi cha Sh200,000 kwa mwezi huku akiishi katika chumba cha 
kupanga, akinunua chakula na mahitaji mengine, akihitaji kusafiri kwenda
 na kurudi kibaruani kwake?
Kwa ufupi, hiki ni kitendawili ambacho 
kinawakabili watu wengi katika nchi hii, wakiwamo wakulima na 
wafanyakazi. Huenda kitendawili hiki kimewaepa wachache wakiwamo 
wafanyabiashara hasa wakubwa ambao hata hivyo ni wachache.
Wakati huu ambao kama si Bunge la Katiba ambalo 
linaendelea mjini Dodoma, watu wengi wangekuwa wameweka macho na masikio
 yao kwenye bajeti ya serikali ambayo kwa kawaida imekuwa ikisomwa mwezi
 Aprili.
Tofauti na miaka michache iliyopita ambako 
matumaini ya wengi yalikuwa ni kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri wa 
Fedha, siku hizi wengi wanaisubiri hotuba hiyo ili kuhesabu ni kiasi 
gani cha maumivu wameongezewa katika maisha yao kwa njia mbalimbali, 
zikiwamo kodi za aina mbalimbali ambazo zimekuwa zikitangazwa kila 
mwaka.
Ukiwauliza watu wengi mijini na vijijini 
watakuambia kuwa afadhali ya jana kuliko leo. Kwa nini? Ni kwa kuwa hali
 ya maisha inazidi kudorora huku hali ya uchumi kwa mtu mmoja mmoja hadi
 kitaifa ikizidi kudhoofika.
Hivyo, kama Taifa, nadhani kuna mambo yamekwenda 
vibaya kiasi kwamba badala ya matumaini ambayo Watanzania wamekuwa 
wakipewa na wanasiasa hasa wakati wa uchaguzi, hali inakuwa kinyume 
chake.
Tatizo ni nini ? Je, kinachoiangusha nchi yetu ni 
sera na mipango mingi ambayo inaandaliwa na wataalamu wetu wakiwamo 
wachumi ambayo utekelezaji wake unategemea zaidi siasa?
Inawezekana kuwa ni kweli kwamba sera na mipango 
mingi inayopangwa kutoka juu kwenda chini badala ya mfumo shirikishi wa 
kuanzia kwenye familia moja, kwenda Serikali za Mitaa na kuendelea kuwa 
juu haufanyiki na badala yake wananchi wote bila kujali tofauti zao za 
kimazingira, jiografia, uchumi wanalazimika kutekeleza sera 
zinazoandaliwa mijini.
Tatizo la mifumo hii ni kwamba wananchi wanalazimika kutekeleza 
mipango mingi ambayo haiwahusishi kwa kiasi kikubwa na matokeo yake 
inapokwama hawana mahali pa kukimbilia.
Ni dhahiri kwamba kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru 
wa nchi hii, wananchi wameendelea kuambiwa maneno na kaulimbiu 
zinazofanana kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Watanzania.
Lakini, je, kilimo hiki cha jembe la mkono ambacho
 si cha kuwezesha kulima na kupata ziada kinaweza kumsaidia vipi 
mwananchi wa Tanzania kujikwamua kimaisha?
Nimesoma mahali kauli ya maaskofu wa Kanisa 
Katoliki Tanzania kupitia baraza lao, TEC ambao wanaeleza kuwa kilimo 
siku hizi ni cha kubabaisha, kibaguzi hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa 
wakulima wameporwa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji, hili ni jambo 
ambalo linaumiza.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment