Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Watu wanaougua ugonjwa wa kisukari wako katika hatari zaidi
kupata magonjwa ya kinywa na meno, kwa sababu sukari ina nafasi kubwa
katika kusababisha magonjwa hayo.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kueleza kuwa asilimia 60 ya
Watanzania wana matatizo ya kinywa na meno.
Akizungumzia uhusiano kati ya kisukari na magonjwa
ya meno, Mtaalamu kutoka Idara ya Sukari Hospitali ya Muhimbili, Dk
Zulfiqarali Abbas alisema ugonjwa wa kisukari huathiri kinga ya mwili,
ambapo baadaye viungo vya mwili huathirika pia.
“Sukari ni adui mkubwa pia wa meno, lazima watu
wapunguze kula sukari na kusafisha meno yao. Hii itawafanya kuwa salama
licha ya kuugua kisukari,” alisema Dk Abbas.
Abbas aliwatoa hofu wagonjwa wa kisukari kuwa dawa
wanazozitumia hazisababishi magonjwa ya kinywa na meno, hivyo
wazingatie kumaliza dawa ili kutibu maradhi yao.
Nao madaktari kutoka Hospitali ya IMTU
wamezungumzia mambo mbalimbali yanayosababisha matatizo hayo, ikiwamo
ulaji mbaya wa vyakula vya sukari na uvutaji wa sigara na unywaji wa
pombe.
Dk. Ally Mzighe alisema watu wamekuwa hawasafishi
vinywa vyao ipasavyo ili kuviweka katika hali ya usafi na kuepuka
bakteria hatari wanaosababisha meno kutoboka, kuvimba fizi na baadaye
kupata kansa.
Mzighe aliwataka wazazi pia kuwa makini katika
kusimamia usafi wa vinywa vya watoto wao, ambao wameanza kuota meno ili
kuwaepusha na bakteria hatari ao.
Naye Dk. Gregory Mandari alisisitiza umuhimu wa
kufanya uchunguzi wa meno mara kwa mara, ili kujua tatizo na kulipatia
ufumbuzi wa haraka .
Dk. Mandari ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya
kinywa na meno katika Hospitali ya IMTU alisema Watanzania wengi hawana
mwamko wa kufanya usafi wa kinywa, matokeo yake huenda hospitali wakati
tatizo limekuwa kubwa.
“Kwa mwezi huwa ninapata watu wawili tu wanaokuja
kufanyiwa uchunguzi meno yao, wengine wengi huja hospitali kung’oa meno
yaliyokwisha toboka na kuathirika sana,” alieleza Dk Mandari.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment