Home » » UPINZANI WAMBANA PROFESA MAGHEMBE

UPINZANI WAMBANA PROFESA MAGHEMBE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe
 
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, imembana Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, baada ya kumtaka ajieleze bungeni zilipo dola za Marekani milioni 284.5 ambazo serikali ya Tanzania ilitakiwa kuzitoa ili kufanikisha awamu ya kwanza ya programu ya uendelezaji wa sekta ya maji nchini.
Msemaji wa wizara hiyo, Magdalena Sakaya (CUF), alitoa msimamo huo wa wapinzani juzi wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo bungeni.
Alisema utekelezaji wa awamu hiyo ya kwanza, ulihitaji Dola za  Marekani milioni 1,691 na kuwa kati ya fedha hizo, Tanzania ilipaswa kutoa Dola milioni 540.2.

“Mwisho wa utekelezaji wa mradi ni mwezi Juni mwaka huu, lakini bado serikali inadaiwa dola za Marekani milioni 284.5 na Watanzania wamebaki gizani kuhusu mradi huu…Sasa tunataka Waziri Maghembe ajieleze mbele ya bunge kwamba hatma ya mradi huu ni nini zaidi ya kufa…Huu ni ubabaishaji ambao hatuwezi kuufumbia macho,” alisema.

Programu hiyo inatekelezwa kupitia miradi midogo minne ambayo ni usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika mabonde tisa, programu ya maji na usafi wa mazingira vijijini, programu ya maji na usafi wa mazingira mijini pamoja na programu ya kuzijengea uwezo na kuimarisha taasisi zinazosimamia na kuratibu programu za maji.

Katika mradi huo, wahisani walichangia Dola za Marekani milioni 1,156.8 na serikali imetoa dola milioni 255.7 kati ya dola milioni 540.2 Kuhusu upotevu wa fedha zaidi ya Sh. milioni 314 katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira -Songea pamoja na limbikizo kubwa la ankara za maji kiasi cha Sh. milioni 147 za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira –Shinyanga, kambi ya upinzani iliitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo.

Sakaya pia alisema Bunge linapaswa kupata ufafanuzi wa taarifa za madai ya mamlaka za maji nchini kushindwa kumudu gharama za ununuzi wa madawa yanayotumiwa kusafisha maji na kuulia wadudu na kisha kusababisha wananchi kutumia maji yasiyo salama.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa