Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katika mfululizo wa makala zangu, nimejikita zaidi katika
kuyachambua magazeti ya Kiswahili kwa lengo la upunguza makosa
yanayojitokeza ama ya kisarufi au ya kifasihi.
Kwa bahati mbaya wanaosoma makala zangu na kuleta
mrejesho ni wasomaji wachache tena ni wa kawaida tu. Hajatokea mwandishi
wa magazeti au hata mhariri anayejali kusoma kwa makini ili kutoa maoni
yake kwa lengo la kuyarekebisha.
Makosa mengi yanajirudia, hata baada ya kuyatolea
ufafanuzi ikiwa ni dalili tosha kuwa waandishi hawasomi na kama wanasoma
hawabadiliki.
Matokeo haya, hayanikatishi tamaa nami nitaendelea na kazi yangu hii.
Mapema mwezi uliopita iliandikwa,
” Shirika hilo lilisema kuwa la kusikitisha zaidi
ni kwamba baadhi ya wavuvi walioathirika ni wahanga wa ghasia za baada
ya uchaguzi mkuu wa 2007.”
Yako maneno mawili yanayotatanisha, nayo ni
wahanga na waathirika. Mhanga ni utoaji wa kafara. Kujitoa mhanga ni
kitendo kinachoweza kuhatarisha maisha kwa ajili ya upigania masilahi
yako au ya mtu mwingine. Athiri ni kutia doa au dosari , jeruhi na
kadhalika.
Kwa hiyo, nomino inayoweza kupatikana kutokana na
kulinyambua neno athiri ni muathiriwa kwa maana ya mtu aliyejeruhiwa au
aliyepata doa au dosari kutokana na kitendo fulani.
Kwa hiyo, siyo sahihi kuwaita walioathirika kuwa ni wahanga.
“ San Kroenke amesaini mkataba wa kuinoa timu hiyo.”
Neno saini limetolewa kutoka katika lugha ya
Kiingereza . Kwa Kiingereza neno hili hutumika kama nomino au kitenzi.
Waswahili walipolikopa neno hili, walipenda kulitumia kama nomino tu na
hadi sasa haya ndiyo matumizi yaliyoenea. Kulitumia vinginevyo,
tunavunja utaratibu uliokubaliwa na wengi.
Badala ya kusaini mkataba, pangetumiwa kutia saini au kuweka saini mkataba.
Kiusahihi ingesomeka, “San Kroenke ametia saini /ameweka saini mkataba mpya wa kuinoa timu hiyo.”
Msomaji mmoja aliwahi kuandika kuwa neno
changamoto linatumika vibaya pamoja na kwamba kisawe chake ni
‘challenge’ kwa lugha ya Kiingereza. Mwandishi aliandika,
“ Wazee wa wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera
watanufaika na ushauri wa kisheria hivyo, kuondokana na changamoto
zinazowakabili katika maisha.”
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), neno changamoto lina maana ya
hamasa, kutia ari, kuwa na hamu ya kufanya jambo. Lilipobadilishwa maana
na kuanza kutumiwa tofauti na maana asilia, linawakanganya wasomaji
wengi. Badala ya kutumia changamoto, yangetolewa maelezo kama ‘baadhi ya
matatizo yanayowakabili.’
Ifahamike kuwa lugha ya mazungumzo ni tofauti kwa
kiasi fulani na lugha ya maandishi. Kwa mfano neno ‘natumai’ linatumika
katika mazungumzo, ila katika uandishi ni sahihi kuandika ‘natumaini’.
Kwa mfano iliandikwa,“ Mwendesha Mashtaka Gerrie Nel alisema kuwa
alitumai kumaliza kumhoji mwana riadha huyo siku ya Jumanne.”
Pamoja na kuandika neno natumai badala ya
natumaini, maneno ‘siku ya Jumanne’ limeandikwa bila sababu ya msingi.
Jumanne ni siku, hivyo haipo haja ya kuongeza neno ‘siku’ ambalo siyo
lazima liandikwe. Kwa usahihi ingeandikwa,“ Mwendesha mashtaka Gerrie
Nel alisema kuwa alitumaini kumaliza kumhoji mwanariadha huyo Jumanne.”
“ Hakika nimehemewa kiasi kwamba nakosa maneno
mazuri ya kuelezea furaha yangu na shukurani zangu kwenu kwa heshima
kubwa mliyonipa.”
Matumizi ya neno ‘hemewa” limetumika isivyo. Kuhemewa maana yake ni kuzongwa na kazi nyingi, kuchoka kutokana na kazi nyingi.
Mhusika alitaka kusema kuwa alizidiwa au alizongwa
na mawazo mengi kiasi kwamba alishingwa kupata maneno ya kutoa shukrani
kwa heshima aliyopewa.
0716 694240
Chanzo;MwananchI
1 comments:
Asante sana. Namijifunza maneno machache kupitia habari hii
Post a Comment