Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Serikali haina mkakati wa kupunguza ajali hizo isipokuwa imejivua jukumu
hilo kwa kuagiza Jeshi la Polisi, Sumatra na Serikali za Mitaa ‘kukaa
pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo’
Hatuna jinsi ya kuelezea masikitiko yetu kutokana na vifo vya
maelfu ya watu vinavyosababishwa na malori katika barabara zetu nchini
kila kukicha. Ni vigumu kupita siku pasipo kusikia ajali za barabarani
zinazotokana na malori ya mizigo. Siku mbili zilizopita, kwa mfano watu
10 walikufa na wengine 15 kujeruhiwa mkoani Mwanza baada ya basi dogo la
abiria kugonga lori la mizigo lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa
barabara.
Hakuna asiyejua kwamba malori katika barabara zetu
ni tatizo kubwa. Wiki iliyopita, gazeti hili lilichapisha habari za
uchunguzi uliofanyika katika sehemu mbalimbali nchini, ukionyesha jinsi
malori mengi yanayosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi,
yanavyosababisha ajali ambazo mpaka sasa zimeua maelfu ya watu, huku
wengine wengi wakiachwa na vilema vya maisha. Inaonekana Serikali
haijatambua ukubwa wa tatizo hilo.
Tunasema hivyo kwa sababu tatu kubwa; kwanza,
ukiichambua hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa wiki
iliyopita bungeni, utagundua kwamba Serikali inalifahamu tatizo la ajali
za barabarani juujuu tu. Imebakia tu kuimba nyimbo zilezile za kuwataka
madereva kuzingatia sheria za barabarani. Pili, takwimu zinazotolewa na
Serikali zimepitwa na wakati na kwa kiasi kikubwa haziendani na takwimu
za Kikosi cha Usalama Barabarani. Tatu, Serikali haina mkakati wa
kupunguza ajali hizo isipokuwa imejivua jukumu hilo kwa kuagiza Jeshi la
Polisi, Sumatra na Serikali za Mitaa ‘kukaa pamoja ili kuweka mkakati
wa kukabiliana na ajali hizo’.
Kwa maneno mengine, Serikali haitambui kwamba
ajali nyingi za barabarani zinazosababisha vifo vya maelfu ya watu
zinasababishwa na malori ya mizigo. Takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya
mwaka 2010 na Machi mwaka huu malori yalisababisha ajali 23,746 na kuua
watu 2,413 na kuacha majeruhi 7,958. Mwaka 2010 pekee, zilitokea ajali
za magari 24,665 na kuua watu 3,582. Kati ya hizo, ajali 3,134
zilisababishwa na malori na kuua watu 493 na kuacha majeruhi 1,926.
Mwaka 2011 kulitokea ajali 33,943 na kuua watu
3,981. Kati ya hizo, zilizosababishwa na malori ni 3,219. Mwaka huo
malori yalisababisha vifo vya watu 506 na kuacha majeruhi 1,792. Wakati
mwaka 2012 zilitokea ajali 33,115 na kuua watu 3,969, kati ya ajali hizo
3,559 zilihusisha malori na kuua watu 692, huku zikiacha majeruhi
1,877. Mwaka 2013 mambo yalikuwa yaleyale, kwani ajali 34,344 zilitokea
na kuua watu 4,002. Kati ya hizo, ajali 3,561 zilisababishwa na malori
na kuua watu 608 na kuacha majeruhi 2,075. Takwimu zinaonyesha pia kuwa,
kati ya Januari na Machi, 2014, ajali 4,893 zimetokea na kuua watu 854.
huku ajali 655 zikisababishwa na malori na kuua watu 114 na majeruhi
288.
Tumetoa takwimu hizo ili kuonyesha jinsi malori ya
mizigo yalivyo janga. Tunaambiwa kwamba wamiliki wake wengi ni vigogo
serikalini na katika sekta ya umma na pengine ndiyo maana usafiri wa
reli ulikufa na juhudi za kuurejesha hazifanikiwi. Serikali inasema ni
sikivu, lakini inashangaza kuona inakuwa kaidi linapokuja suala la
kudhibiti malori hayo. Wakati tukisubiri kufufuliwa kwa usafiri wa reli,
tunaishauri Serikali ijenge na kutenga sehemu maalumu za kuegesha
magari hayo katika miji na barabara zote kuu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment