Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Inaadhimishwa nchini kote kuanzia ngazi ya wilaya hadi
Taifa. Ni wiki inayowakutanisha pamoja wadau kujadili maendeleo ya Sekta
ya Elimu
Ni tukio la kwanza la aina yake nchini
litakaloshuhudia wadau muhimu wa elimu wakipongezwa kwa mafanikio yao
katika kuiendeleza Sekta ya Elimu.
Katika wiki hii, iliyoanza Mei 3 na ambayo
itahitimishwa kitaifa Mei 10, harakati zake zinaelezwa kuanzia katika
ngazi za halmashauri, mkoa na hatimaye taifa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru
Kawambwa anasema, pamoja na mambo mengine, Wiki ya Elimu inalenga
kuunganisha nguvu na mawazo ya wadau kuelekea upatikanaji wa elimu bora.
“Lengo la kuwa na Wiki ya Elimu ambayo itakuwa
ikiadhimishwa kila mwaka, ni kuelimisha umma juu ya umuhimu wa elimu
bora na kuhamasishana kuchochea ari ya ushindani wa kitaaluma kwa wadau
mbalimbali wa elimu, wakiwamo walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa
jumla,” anasema .
“Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Elimu Bora kwa Wote Inawezekana, Timiza Wajibu Wako’.”
Wasaa wa tafakuri
Meneja mawasiliano na utetezi katika Ofisi ya
Rais, Usimamiaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB), Hassan Abbas anasema
Wiki ya Elimu ni wasaa mzuri kwa wananchi kufanya tafakuri ya safari ya
kuboresha elimu yao.
“Ni kipindi cha tafakuri kwa sababu sote
tunafahamu kuwa elimu bora ndio ukombozi wa Taifa hili katika kutoa
wataalamu wa nyanja na fani mbalimbali,’’ anaeleza.
Ni dhahiri kuwa kila mtu angependa kuona nchi
inapiga hatua kubwa ya mafanikio katika njanja zote. Mafanikio hayo
yatatokana na mfumo mzuri wa elimu unaotoa wahitimu wenye stadi muhimu
na sahihi.
Abbas anaongeza: “Wiki ya Elimu inatupa fursa
maridhawa kwa sote kujiuliza tunafanya nini katika kufikia elimu bora,
ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuifafanua kuwa ni ile inayompa
mtu stadi muhimu za kuyamudu maisha yake.
“Ni dhahiri kuwa kila mmoja wetu ana kitu cha
kuchangia. Hivyo lengo la wiki hii litatimia iwapo kila mhusika
atachangia mawazo yake katika kuboresha sekta ya elimu. ‘’
Tuzo na motisha
Sambamba na mijadala kuhusu mustakabali wa elimu,
Wiki ya Elimu itatumika kutoa tuzo kwa halmashauri, shule na wanafunzi
waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa mwaka jana.
Ofisa elimu mkuu katika Kitengo cha Usimamizi wa
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Hilda Mkandawile anasema tuzo itakuwa za
fedha na zisizo za fedha.
Anasema tuzo hizo zitatolewa katika makundi matano
ambayo ni shule zilizofanya vizuri katika mtihani wa mwaka 2013 na
zilizoonyesha maendeleo ya juu kwa kulinganisha matokeo ya mwaka 2012
na 2013.
Makundi mengine ni wanafunzi waliofanya vizuri
katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari mwaka 2013, na
Mkoa na Halmashauri iliyofanya vizuri katika taaluma.
Pia kutakuwa na tuzo kwa wanafunzi walioshinda
katika mashindano ya insha za jumuiya ya SADC na Open Goverment
Partnership (OGP).
Mafanikio ya Mpango wa GRN
Kupitia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa (GRN) ulioanza mwezi Aprili mwaka jana, Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi na vyombo inavyovisimamia inajivunia mafanikio kadhaa ya kutia
moyo katika sekta ya elimu.
Kwa mfano, mkakati wa kuzipanga shule kitaifa kwa
kuzingatia ubora wa ufaulu wa shule katika mtihani, umeleta hamasa kubwa
na kukuza ari ya wadau wa shule kuhakikisha shule zao zinafanya vizuri
hivyo kupanda daraja la ufaulu kitaifa, kwa mujibub wa kaimu katibu
mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde.
“Baraza la Mitihani limeandaa vitabu vya mwongozo
wa upangaji wa shule katika makundi ya ufaulu kwa madhumuni ya
kuwawezesha wadau wote wa elimu kufahamu jinsi upangaji wa shule kwa
ubora wa ufaulu unavyofanywa,’’ anafafanua.
Mafanikio mengine anayotaja Dk Msonde ni kufanya
upembuzi wa kubaini makosa yanayofanywa na watahiniwa na kutoa mwongozo
kwa wadau kama sehemu ya kukabiliana na tatizo la watahiniwa kutojibu
maswali ipasavyo.
“ Baraza limeandaa na kusambaza kwa wadau wa elimu
vitabu vya uchambuzi wa ufaulu wa watahiniwa kwa kila swali kwa shule
za msingi na sekondari kwa masomo yote, ili walimu na wanafunzi waweze
kufahamu changamoto zilizopo wakati wa kujibu maswali ya mitihani,
hivyo kujifunza mbinu bora za kujibu maswali,’’ anaeleza.
Wizara pia imejifunga kibwebwe ikishupalia kupunguza na kumaliza
tatizo la wanafunzi wa shule za msingi, wakiwamo wahitimu wa darasa la
saba kushindwa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara inatekeleza
mkakati wa Upimaji wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) wenye
lengo la kuwapima wanafunzi kwa ngazi ya shule na kitaifa kuhusu
kumudu stadi hizo.
Kaimu mkurugenzi wa Elimu ya Msingi, Sara Mlaki
anasema upimaji wa kitaifa wa stadi za KKK ulifanyika Julai mwaka 2013
kwa kutumia zana za kimataifa kwa lengo la kufuatilia viwango
vilivyofikiwa na wanafunzi katika shule za msingi kuhusu stadi za
kusoma, kuandika na ufanyaji wa hesabu. Jumla ya wanafunzi 2,266 kutoka
shule 200 na Halmashauri 20 walishiriki katika upimaji huo.
Akizungumzia matokeo, Mlaki anasema asilimia 40
ya wanafunzi hawakuweza kujibu angalau swali moja kwa ufasaha na
asilimia 8 ya wanafunzi wa darasa la pili walikuwa wakisoma na kuelewa.
Kuhusu tathmini ya kusoma Kiingereza, ilionyesha
kuwa watoto wanajifunza Kiingereza kwa mara ya kwanza wakiwa darasa la
pili na wanajifunza kama somo, hivyo siyo jambo la kushangaza kwamba
baada ya mwaka mmoja bado watoto wengi wanakosa ufahamu wa lugha hiyo.
“Tathmini ya Hisabati ilibainisha kwamba wanafunzi
wanafanya vizuri zaidi katika maarifa ya akili (wanakumbuka) vitu,
lakini hawafanyi vizuri katika maswali ya kuelewa zaidi na kutumia
maarifa yao ya kiakili, huku mkazo wa ufundishaji wa somo hilo ukizama
zaidi katika kukariri vipengele na kanuni,’’ anaeleza Mlaki.
Matokeo ya tathmini hii bila shaka yanashadadia
ukweli kuwa KKK bado ni changamoto tete katika mfumo wa elimu. Hili ni
moja ya matatizo lukuki yanayopaswa kufanyiwa tafakuri ya kina na wadau
wa elimu hasa katika wiki hii ya elimu.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment