Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, Bw.
Moses Machali (NCCR-Mageuzi), anadaiwa kumpiga baba yake mzazi Mzee
Joseph Machali kwa madai ya kutaka kumrekebisha tabia akidai kuchoshwa
na kitendo chake cha kulewa pombe kupindukia.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi ambapo
mbunge huyo pia inadaiwa alimfukuza baba yake nyumbani na kumtupia nguo
zake nje ambapo kutokana na kipigo hicho, Mzee huyo alikimbilia kwa
mjumbe wa nyumba 10 aliyefahamika kwa jina la Dickson Joaqim.
Hatua hiyo imefuatia baada ya kuchoshwa na
tabia hiyo na hivyo kuamua kumpatia kichapo hicho kwa lengo la
kumrekebisha tabia jambo ambalo limesababisha kumpatia maumivu ya
kutenguka kwa mkono.
Anadaiwa kuwa, siku ya tukio Mzee huyo
alichelewa kurudi nyumbani na alipomgongea mwanaye (Mbunge Machali),
alimfungulia na kuanza kumshushia kipigo hicho baada ya kuchoshwa na
tabia yake.
Ili kuthibitisha madai hayo, Mwandishi wetu
aliyepo mkoani Kigoma, alimpigia simu Bw. Machali ambaye alikiri kufanya
tukio hilo na kudai kuwa, mzazi wake ana tabia ya kunywa pombe
kupindukia hivyo kumuathiri yeye kisiasa anapowajibika kwa wananchi
wake.
"Sikuwa na nia ya kufikia hatua ya kumpiga
Mzee wangu, najitambua ndiyo maana namsihi aachane na pombe...najisikia
vibaya kuona analewa, tukiwekana sawa, baadhi ya watu wanadai nampangia
sheria," alisema.
Alisema kuanzia sasa, atakuwa sambamba na Mzee wake ambaye
baada ya kipigo hicho, alifungua kesi polisi lakini amekubali kuifuta na kwenda kulimaliza suala hilo kifamilia.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walidai
kumuona Mzee huyo akiwa na fomu namba tatu ya matibabu inayotolewa na
polisi (PF3) ambayo imemwezesha kupatiwa matibabu katika moja ya
zahanati wilayani hapo.
Chumba cha habari Majira, kilifanya jitihada
za kumpigia simu Bw. Machali ili aweze kuzungumzia tukio hilo kwa
undani ambapo awali simu yake ilikuwa ikitumika na baadaye alizimwa
kabisa.
Baada ya kumkosa Bw. Machali, Majira
liliwasiliana kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Frasser
Kashai ambaye alithibitisha jeshi hilo kupokea taarifa za Mzee Machali.
Alisema baada ya Mzee Machali kupeleka
malalamiko ya kupigwa na mtoto wake, jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata
Bw. Machali na kumhoji ambapo jana ilikuwa apelekwe mahakamani kujibu
mashtaka.
"Tukiwa kwenye harakati za kutaka kumpeleka
mahakamani kwa tuhuma za kumpiga baba yake, mlalamikaji ambaye ni Mzee
Machali aliomba kesi hii ifutwe ili wakalizungumzie suala hili nyumbani
kifamilia," alisema
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment