Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MENEJA wa Mfuko wa Bima ya afya Mkoa wa Kigoma (NHIF), Elias
Odhiambo amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kujiunga na bima ya
afya ili kuondokana na hofu ya kukosa matibabu wanapoumwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za Chama cha
Waandishi wa Habari Mkoa wa Kigoma (KGPC), Meneja huyo alisema kuwa,
gharama ya kujiunga na mfuko huo kwa vikundi au taasisi isiyo ya
serikali ni sh 76,300 kwa kila mwanachama, ambako atapata matibabu kwa
mwaka mzima kwa fedha hiyo.
”Hivi sasa gharama za matibabu kwa kweli zipo juu sana, hivyo ni
wakati wa kuangalia mnaelekea wapi, kujiunga na bima ya afya ni suala
la msingi ili kuwa na uhakika wa matibabu unapougua, kwani unaweza
kuugua kipindi ambacho huna hata pesa mfukoni, mtafakari vizuri na
kufanya maamuzi,” alisema Odhiambo.
Meneja huyo alisema, huduma zinazotolewa na NHIF ni bora zaidi, kwani
zinampa mwanachama uhuru wa kuchagua mahali au kituo anachopenda
kupata huduma ya matibabu.
Alisema, hadi sasa NHIF imesajili vituo vya afya na maduka ya dawa
5,840 kwa nchi nzima, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa
wananchama.
Naye Mwenyekiti wa KGPC, Deogratius Nsokolo, alisema, wanachama wake
watajiunga na mfuko huo kwa kuwa una manufaa makubwa na wataishawishi
jamii kujiunga na mfuko huo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment