Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kutumia fursa
waliyoipata ya maonyesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati Kanda ya
Kati kwa kujitangaza kibiashara na kujifunza kutoka kwa wenzao ndani na
nje ya nchi.
Akizungumza mjini hapa jana katika kikao kilichohusisha viongozi wa
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (Sido), na Waandishi wa
Habari, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu Issa Machibya, alisema
maonyesho hayo yatafanyika Community Centre kuanzia Agosti 27 hadi
Septemba Mosi na kujumuisha mikoa mbalimbali ya hapa nchini pamoja na
nchi za Kenya, Uganda, DRC na Burundi.
Alisema kuwa maonyesho hayo hufanyika kwa mwaka mara moja nchini na
mwaka huu Mkoa wa Kigoma umepata nafasi hiyo, hivyo wananchi wanatakiwa
kutumia fursa hiyo kujitangaza na kujifunza, kwani itachukua miaka
mingi kujirudia tena.
Machibya, alisema kutakuwepo na waonyeshaji 302 ambao wamethibitisha
kushiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi, pia
Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zitakuwepo kama TBS, NMB,
Tanapa, Benki ya Posta na nyinginezo.
Aliongeza kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwawezesha wajasiriamali
wadogo wa hapa nchini, kupata fursa ya kukuza soko la bidhaa zao
hususan mikoa ya kanda ya kati na nje ya nchi, pamoja na kujifunza
kutoka kwa wenzao wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Machibya aliongeza kuwa kauli mbiu ya maonyesho hayo ni ‘Buni, Boresha, Fanya Biashara Kupitia Sido’.
Naye Meneja wa Sido mkoani hapa, Macdonard Maganga, alisema pamoja
na wajasiriamali kuja katika maonyesho hayo kwa lengo la kuonyesha
bidhaa zao, lakini pia ni fursa nzuri kwa wananchi wa hapa nchini
kujitangaza, pia kuchukua ujuzi kutoka kwa wageni.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment