Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katika makala iliyopita tuliangalia baadhi ya sifa anazotakiwa
kuwa nazo mwalimu. Katika makala haya tutaendelea na sifa nyingine.
Moja kati ya sifa kubwa ambayo mwalimu anatakiwa
kuwa nayo ni ushirikiano kati yake na walimu wenzake, wanafunzi na
wazazi kwa jumla.
Ushirikiano na walimu wenzake utamwezesha kufanya kazi yake vizuri, lakini pia kuboresha upeo wa fikra na taaluma kwa jumla.
Ama kwa upande wa wanafunzi, ushirikiano utaondoa
kizuizi kati yake na wanafunzi na utawaweka huru wanafunzi kuweza
kumhusisha pale wanapokuwa na matatizo mbalimbali.
Wazazi pia wanatakiwa washirikishwe katika kujua
maendeleo ya watoto wao shuleni. Katika kufanikisha hili mwalimu ana
nafasi kubwa.
Pia, mwalimu anatakiwa awe muumini mkubwa wa
nidhamu. Mwalimu anatakiwa asifumbie macho vitendo vya utovu wa nidhamu
miongoni mwa wanafunzi na avikemee bila kupepesa macho.
Hivi sasa kuna changamoto kubwa katika kudhibiti
nidhamu za wanafunzi ukizingatia kuwa adhabu ya viboko imekatazwa
shuleni. Lakini pamoja na kukatazwa huku kwa adhabu ya viboko bado
mwalimu ana wajibu wa kutumia mbinu mbadala katika kudhibiti nidhamu za
wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa nidhamu ni nyenzo muhimu katika
maendeleo ya taaluma. Katika kudhibiti nidhamu mwalimu anatakiwa yeye
mwenyewe ajiheshimu. Haipendezi kumwona mwalimu akiwa amevaa mavazi
yasiyo na stara yanayoonesha utupu kwa wanawake au kuvaa mlegezo kwa
wanaume.
Pia, kujichora katika mwili au kuvuta bangi na
dawa za kulevya. Huwezi kudhibiti nidhamu za wanafunzi kama wewe
mwenyewe hujiheshimu.
Mwalimu hatakiwi kuwa mwoga na kuogopa kukosolewa
katika masuala yanayohusu taaluma. Uthubutu ni katika sifa zilizotukuka
za mwalimu. Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa ziada wa kuchagiza
maendeleo ya wanafunzi na kutatua matatizo mbalimbali yanayohusu taaluma
na wanafunzi kwa jumla.
Anatakiwa awape moyo wanafunzi wake nao wajifunze kutoka kwake ili waweze kufanikiwa kitaaluma na kimaisha.
Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa kuwahusisha
wanafunzi wake ili waweze kufuatilia masomo darasani. Wanafunzi wana
maarifa mbalimbali ambayo mwalimu pia anaweza kunufaika nayo akitaka.
Usiwachukulie wanafunzi wako kama watu wasio na kitu kichwani na
usitawale darasa kana kwamba wewe ndiye mjuzi wa kila jambo.
Washirikishe na wajengee wanafunzi wako uwezo wa kujiamini na kutenda na
huu ndiyo msingi mkubwa katika maendeleo ya taaluma.
Kuwa na moyo wa huruma na kusamehe ni sifa
iliyotukuka ya mwalimu. Mwalimu si mtu wa kuendekeza malumbano yasiyo na
tija kwa wanafunzi wake na walimu wengine. Mazingira ya amani na
utulivu shuleni ni muhimu kwa maendeleo ya taaluma.
Sifa ni nyingi, lakini ningependa tutosheke na
hizi chache ambazo zinaweza kuwakumbusha walimu thamani yao na umuhimu
wao katika kuendeleza taaluma.
Ni vizuri nikiwakumbusha walimu kuwa ualimu ni
mojawapo ya kazi tukufu kabisa katika historia ya mwanadamu na hakuna
jamii yoyote iliyofanikiwa bila ya kuwa na walimu bora.
Hivyo, pamoja na changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo, wajithamini na watambue kuwa wana mchango mkubwa
katika kuikomboa jamii kutokana na adui ujinga na hatimaye kuiletea
maendeleo.
Rajabu Kipango ni mwalimu na mtaalamu wa rasilimali watu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment