Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADHI ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wametaka kuongezwa kwa huduma za malipo ya nauli na posho kwa wanachama wanaokwenda kwenye matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao, sambamba na kugharamia upimaji wa vinasaba (DNA).
Walisema hayo walipozungumza wakati wa kikao cha pamoja baina ya wanachama wa mfuko huo katika kijiji cha Mwamgongo, Kigoma Vijijini mkoani hapa na viongozi wa mkoa wa mfuko huo.
Walisema kuwa ni vizuri wanachama wanaokwenda kupata matibabu ya rufaa, wagharamiwe nauli na posho na mfuko huo.
Nassib Ally, mtumishi katika Kituo cha Afya cha Mwamgongo, alisema licha ya sasa malipo ya nauli na posho za safari kulipwa na mwajiri, lakini wakati mwingine malipo hayo hayalipwi kwa wakati.
Alisema hali hiyo huwafanya wanachama kuhangaika kufuatilia matibabu ya rufaa nje ya vituo vyao vya kazi.
Mussa Boniface, mwalimu wa Shule ya Msingi Mwamgongo, alitaka mfuko kugharamia huduma za upimaji wa DNA na kugharamia huduma za matibabu ya nje ya nchi kwa wanachama wake.
Akizungumzia maombi hayo, Meneja wa NHIF mkoa wa Kigoma, Elius Odhiambo alisema kwa sasa mfuko haugharamii malipo ya posho na nauli kwa wanachama wake, wanaokwenda rufaa nje ya vituo vya kazi. Alieleza kwamba suala hilo litabaki kuwa juu ya mwajiri.
Odhiambo alisema kitendo cha kugharamia posho na nauli kwa wanachama, itawalazimu wanachama hao kuchangia zaidi.
Alieleza kwamba suala hilo linahitaji mjadala mrefu ambao utaridhiwa na wanachama wote kuweza kutekeleza hilo.
Meneja huyo pia alisema suala la maombi ya mfuko kugharamia matibabu ya nje ya nchi, litabaki chini ya wizara ya afya huku upimaji wa vinasaba ukiendelea kuwa gharama za mtu binafsi.
Chanzo;Habari leo
0 comments:
Post a Comment