Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAMLAKA ya Chakula Dawa na Vipodozi nchini (TFDA), imetoa amri ya
kufungwa kwa machinjio ya Kibirizi endapo haitafanyiwa marekebisho huku
ile ya Ujiji ikifungiwa kutokana na kutokukidhi vigezo vinavyotakiwa
kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za afya ya mwaka 2003.
Hatua hiyo imetokana na ziara ya mamlaka kuona upungufu uliyopo,
ambako kuna uwezekano mkubwa wa kusababisha athari za kiafya kwa
wananchi kutokana na magonjwa ya mlipuko.
Akitolea ufafanuzi hatua hiyo, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi
ambaye pia ni Mganga wa Mifugo, Dk. John Shauri, alisema hatua hiyo
imechukuliwa Septemba 15 mwaka huu baada ya kubaini upungufu na kutoa
onyo la kutotumika hadi hapo marekebisho yatakapofanyika.
Alitaja baadhi ya sababu zilizosababisha kufungwa kwa machinjio ya
Ujiji kuwa ni pamoja na kuchakaa kwa jengo, kutuama kwa maji katika
sakafu kutokana na mashimo, kutokuwepo kwa uzio, kukosekana kwa shimo la
kutupia nyama iliyozuiliwa kutumiwa, kutokuwepo kwa choo pamoja na
maji.
“Kutokana na vigezo hivyo kutokuonekana pale, wao kama mamlaka
iliyopewa jukumu la kisheria wamefunga machinjio yale kuendelea
kutumika hadi pale yatakapojengwa upya kwa kuzingatia vigezo
vinavyotakiwa kitaalamu kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2003,” alisema
Dk. Shauri.
Aidha, Shauri akitolea ufafanuzi machinjio ya Kibirizi, alisema
kutokana na kasoro ndogo ndogo zilizopo ikiwemo uzio, ilitolewa amri ya
kufanyiwa marekebisho ya haraka ili wananchi waendelee kupata huduma ya
mboga kama kawaida.
“Machinjio ya Kibirizi yaliachwa kwa sababu mapungufu yake yalikuwa
madogo ukilinganisha na machinjio ya Ujiji, ambayo yana mapungufu mengi
na tayari uzio umeshawekwa ili kuzuia mbwa na wanyama wengine wasiingie
sambamba na marekebisho mengine,” alisema.
Naye Laini Ramadhani, ambaye ni wakala wa usambazaji wa nyama,
alisema kuwa kufungwa kwa machinjio ya Ujiji hakuna haki iliyotendeka,
kwani imekuwa ghafla na cha kushangaza ni kuacha eneo la Kibirizi
kuendelea kufanya kazi na wakati mazingira yanafanana.
“Kama wanafuata haki… basi wangetoa barua kabla ya kuja kufunga ili
sisi tujue cha kufanya baada ya kufungwa na kutafuta namna ya
kurekebisha mapungufu yanayoonekana,” alisema Ramadhani.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnazi Mmoja ambako machinjio ya
Ujiji inapatikana, Nuru Sadiki, alisema anaunga mkono kufungwa kwa
machinjio hiyo kutokana na kukosa sifa za usafi.
“Kutokana na mapungufu mengi yaliyoko katika machinjio hii, ilikuwa
ni lazima ifungwe kwani hatuko tayari kuona wananchi wakipata magonjwa,
pia hata ile ya Kibirizi kama nayo ina hali hii basi nayo inatakiwa
kufungwa ili kupisha marekebisho ambayo yatawafanya wananchi kupata
nyama iliyotoka katika mazingira masafi” alisema Sadiki.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment