Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU watatu wamefariki dunia na wengine hawajulikani walipo baada ya kuibuka mapigano ya kugombania ardhi yaliyowahusisha wafugaji na wakulima katika Kijiji cha Minyinya Kata ya Nyamtukuza Wilaya ya Kakonko mkoani hapa.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Justini Kilegea, alisema mapigano hayo yalitokea usiku wa kuamkia juzi baada watu jamii ya wafugaji wanaoishi mashambani, kuvamia nyumba za wakulima na kuzusha vurugu kwa kuzichoma na kuuwa watu wawili.
Alisema kuwa, mapigano hayo yalihusishwa na ulipizaji kisasi baada ya Oktoba 15, watu wasiojulikana kumuua mtu mmoja jamii ya wafugaji na kukatakata ng’ombe wake, kitendo kilichowafanya wafugaji kulipa kisasi kwa kufanya vurugu hizo na kusababisha mauaji ya wakulima wawili.
“Watu waliouwawa ni Kachila Kahegele mwenye miaka 28 na Lameck Kachila mwenye miaka 26 wote wakiwa wanaume,” alisema Kilegea.
Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Venance Mwamoto na Kamati ya Ulinzi na Usalama walifika katika kijiji hicho ili kuona hali halisi ilivyo, na kuwataka wananchi kuacha kushambuliana na kulipizana visasi, kwani hali hiyo ni hatari na inahatarisha amani.
Pia, aliwataka wanasiasa kutoliingilia suala hilo kisisa bali wote wanatakiwa kushirikiana kuweza kutatua matatizo yao ili jamii iishi kwa amani na utulivu.
chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment