Na Joseph Ishengoma,
MAELEZO
26/11/2015
Askofu Mkuu wa jimbo
kuu la Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka kesho (tarehe 27.11.2015) anatarajia kuongoza
ujumbe wa Tanzania kwenye ziara ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Baba
Mtakatifu Francis nchini Uganda.
Baba Mtakatifu Francis
anatarajia kuwasili nchini Uganda kesho kwa ziara ya siku mbili akitokea Kenya
kabla ya kuelekea Afrika ya Kati.
Hii ni ziara ya
kwanza kwa kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kutembelea Bara la
Afrika tangu alipoliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013.
Katibu wa Baraza la
Maaskofu (TEC) nchini Padre Raymond Saba amesema Mabaraza ya Maaskofu ya Kenya na Uganda kwa
pamoja yalitoa mwaliko kwa TEC kushiriki katika ziara ya Baba Mtakatifu katika
nchi hizo.
“Tulipata mwaliko
kutoka Kenya na Uganda, lakini tumeangalia nafasi yetu na jinsi ya kushiriki
katika ziara hii. Hatukuweza kutuma mwakilishi Kenya, lakini Askofu Ruzoka
ataiwakilisha TEC Uganda,” amesema.
Kwa mujibu wa msemaji
huyo, jana mabasi mawili ya waumini wa dini ya Kikristo yaliondoka mjini Mwanza
kuelekea Namugongo, Uganda ambapo Baba Mtakatifu atakapofanyia ibada.
Eneo la Namugongo
ndipo Mfalme Kabaka Mwanga II alipowachoma na kuwaua mashahidi 22 wa Uganda waliofia
dini katika karne ya 18.
“Natoa wito kwa
waumini wa Kanisa Katoliki nchini, wafuatilie na kusikiliza kwa makini ujumbe
wa Baba Mtakatifu aliouleta katika Barani Afrika kwa sababu unagusa moja kwa
moja amani na ushirikiano miongoni mwa jamii,” amesema.
Kwa mujibu wa Padre
Saba, Baba Mtakatifu hufanya ziara kufuatia mwaliko wa kanisa na serikali ya mahali
husika au tukio la kimataifa linalohusiana na imani Katoliki.
Amesema, “Kanisa pekee
yake haliwezi kufanikisha ziara ya Baba Mtakatifu. Ndio maana alipofika Kenya
alipokelewa na Rais Uhuru Kenyatta na hata alipokuwa Marekani alipokelewa na
Rais Baraka Obama ingawa sio rahisi kwa kiongozi wa Marekani kumpokea mgeni
uwanja wa ndege.”
Ziara ya Baba
mtakatifu nchini Marekani ilipangwa kabla hajawa kiongozi Mkuu wa kanisa
Katoliki. Ziara hiyo ilitokana na kongamano la kimataifa la familia lililofanyika
mjini Filadelphia.
Papa Francis
anatarajia kuhudhulia kongamano la vijana ulimwenguni nchini Poland mwaka 2016.
0 comments:
Post a Comment