Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI wilayani Uvinza mkoani Kigoma imetangaza kuwachukulia hatua
viongozi wa vijiji watakaoshindwa kutekeleza malengo yaliyowekwa katika
kusimamia uhamasishaji wa jamii kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF).
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo alisema hayo akifunga kikao
cha wadau kilichokuwa kikijadili mchakato wa upitishaji wa sheria ndogo
ya Halmashauri ya kutambua na kusimamia utekelezaji wa huduma za mfuko
wa afya ya jamii na bodi za afya katika wilaya hiyo.
Gambo alisema baada ya kikao hicho mkakati uliopo ni kuhakikisha
wananchi wote wa wilaya hiyo wanajiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ambapo
vijiji vimepewa malengo ya uandikishaji wa asilimia 80 kwa kaya huku
watendaji wa vijiji wakiwa ndiyo wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa
mpango huo.
Alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wajumbe wa
bodi za usimamizi wa afya katika ngazi za kata na wilaya watakaoshindwa
kusimamia utoaji huduma bora za afya katika maeneo yao kwa huduma hizo
kugubikwa na malalamiko ya wananchi ikiwemo wizi wa dawa na kauli za
unyanyasaji za watoa huduma.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), Ally Mwakababu kutoka mkoani Tanga alisema changamoto kubwa kwa
sasa katika utoaji huduma kwenye sekta ya afya ni dawa, vitendea kazi na
wataalamu.
Mwakababu alisema kujiunga kwa wingi kwa jamii katika NHIF na tiba
kwa kadi kutawezesha halmashauri kutumia fedha inazopata katika
kukabiliana na changamoto hizo na hivyo kuwezesha wananchi wanaotoa
fedha zao kupata huduma bora wakati wote.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Uvinza, Omari Mkombole alisema kwa sasa hali ya uchangiaji wa
wananchi katika CHF wilayani humo iko chini na sababu kubwa ni
changamoto zilizopo kwenye utoaji huduma, hali ambayo baada ya mkutano
huo mkakati umewekwa kuhakikisha asilimia 80 ya kaya 70,000 zenye jumla
ya watu 400,000 zinajiunga na Mfuko huo.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment