KIONGOZI wa chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe
Zitto, anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wabunge kutoka nchi tofauti
duniani ulioandaliwa na Benki ya Dunia nchini Marekani.
Kwenye mkutano huo, Zitto atatoa mada kuhusu masuala ya hifadhi ya
jamii kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi. Pia atahudhuria kozi
maalumu ya uongozi katika Chuo Kikuu cha Harvard, nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson
Mwigamba, ilieleza kuwa Zitto atakuwa nje ya nchi kuanzia jana, Aprili 7
hadi Aprili 29 mwaka huu kwa shughuli mbalimbali ikiwamo kuhudhuria
mkutano huo.
“Kutokana na safari hiyo na kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo ya
mwaka 2015, Ibara ya 29 ibara ndogo ya (25) kipengele cha (xi), Kiongozi
wa Chama amemteua Yeremia Kulwa Maganja ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge na Serikali za Mitaa Taifa, kukaimu nafasi ya Kiongozi wa chama
kwa muda ambao hatakuwepo nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mwigamba alisema, katika taarifa hiyo kuwa, uongozi na Mwenyekiti wa
chama hicho wanamtakia Maganja utekelezaji bora wa majukumu yake kwa
kipindi hicho.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment