Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa
Serikali imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL)
kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ili
kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki kabla ya
maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa,
alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki mkoani Kigoma, wakati akikagua
miundombinu ya reli na kusisitiza nia ya serikali kufufua reli ya Kanda
ya Kaskazini ili kuimarisha huduma za uchukuzi katika mikoa ya Tanga,
Kilimanjaro na Arusha.
“Kama serikali tumewekeza vya kutosha katika TRL, hivyo tunawataka
mfanye biashara itakayolipa nasi tutahakikisha popote reli ilipo inatoa
huduma iliyokusudiwa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi," alisema.
Aidha, Prof. Mbarawa aliwataka wafanyakazi wa TRL kufanya kazi kwa
bidii na uadilifu ili kupata bidhaa na abiria wengi wa kuwasafirisha
nchini kote.
Alisema serikali imedhamiria kuiongezea nguvu TRL na kwamba baadhi
ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
itakabidhiwa kwa shirika hilo, hivyo kulitaka kuwa na mpango madhubuti
wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya usafiri wa reli hapa nchini.
“Fanyeni bidii ili mpate mizigo ya kusafirisha kutoka Tanga kwenda
Moshi na Arusha ili kufikia lengo la kubeba mizigo tani milioni moja kwa
mwaka,” alihimiza. Prof. Mbarawa pia alizungumzia umuhimu wa TRL
kufanyakazi kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), ili
kuongeza kasi ya huduma za uchukuzi nchini, kuongeza fursa za ajira na
kukuza pato la shirika na taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Masanja Kadogosa, alisema
shirika hilo limejipanga kutafuta masoko ndani na nje ya nchi ili
kuboresha huduma za uchukuzi na kukuza pato lake.
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alikagua Meli ya MV Liemba na
kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra), kuhakikisha meli za MV Liemba na MV Mwongozo zinakaguliwa na
kufanya kazi inavyostahili katika Ziwa la Tanganyika.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment