ENEO la ardhi oevu la Malagarasi liko hatarini kutoweka kutokana na
ongezeko kubwa la matumizi ya ardhi na maji linalosababisha uharibifu wa
mazingira.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji katika bonde hilo
uliofanyika mjini Kigoma hivi karibuni Meneja wa Bonde la Maji la Ziwa
Tanganyika, Chobariko Rubwabwa, mpango mkakati unahitajika kwa haraka
ili kunusuru eneo hilo.
Rubwabwa alisema kuwa utafiti unaonesha kuwa kwa sasa eneo hilo la
ardhi oevu ya Malagarasi limeelemewa na matumizi makubwa ya watu na
uharibifu wa mazingira.
Alisema ifikapo mwaka 2020, hali itakuwa mbaya zaidi kama hatua hazitachukuliwa sasa.
Rubwabwa alisema ongezeko kubwa la watu kuzunguka eneo hilo, ongezeko
la matumizi ya shughuli za binadamu ikiwamo kilimo na ufugaji na
uharibifu mkubwa wa mazingira ni miongoni mwa athari zinazotishiwa
kutoweka kwa eneo hilo.
Alisema kuwa kwa sasa eneo la ardhi oevu ya Malagarasi linakabiliwa
na msongo wa maji kutokana na matumizi ya maji hayo kutotosheleza
mahitaji huku matumizi yakiwa makubwa sambamba na uanzishwaji wa miradi
mikubwa ya kilimo.
Alisema taarifa za utafiti na ushauri wa kitaaluma unaotolewa haufanyiwi kazi vya kutosha na Halmashauri husika.
Akizungumzia hali hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Emmanuel Kalebero, alisema kuanzia sasa ni lazima ofisi za
mabonde ya maji nchini yaridhie na kutoa kibali kwa matumizi yoyote ya
maji na maeneo yanayotaka kufanyika kwenye maeneo ya mabonde nchi.
Kalebero alisema ongezeko kubwa la watu na ongezeko kubwa la matumizi
ya mabonde ni lazima yafanyiwe tathmini na ofisi za mabonde kuona
mipango ya matumizi endelevu ya miradi inayotaka kufanyika sambamba na
utunzaji wa mazingira ya maeneo hayo.
Alisema kuwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameyakumba maeneo ya
mabonde nchini yanatokana na matumizi holela ya maeneo hayo na uharibifu
mkubwa wa mazingira yamefanya kupungua kwa kiwango cha maji katika
mabonde mbalimbali nchini.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment