Home » » Miaka tisa ya kugombea ardhi Kigoma na kukwama huduma za kipindupindu

Miaka tisa ya kugombea ardhi Kigoma na kukwama huduma za kipindupindu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Hali ya ndani ya Kituo cha Kupambana na Kipindupindu cha Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
MAENDELEO ya Kituo cha Afya cha Gungu katika kata ya Kikungu iliyoko katika Manispaa ya Ujiji, mkoani Kigoma, yameingia utata kutokana na mgogoro wa ardhi unaoIkabili.


Ni takriban miaka tisa sasa uongozi wa kituo hicho cha afya, umeshindwa kuendelezwa miundombinu yake, ikiwamo kujenga uzio na kuanzisha kituo cha kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu wilayani na sehemu ya kupumzikia wagonjwa.
Mgogoro mkuu umejikita katika kugombea ardhi kati ya Manispaa ya Ujiji/ Kigoma na taasisi binafsi inayodai kumiliki eneo hilo.
Mwandishi wa makala alishuhudia mgogoro huo wakati alipotembelea wilaya hiyo hivi karibuni na kupata fursa ya kuzungumza na pande mbili zinazohusika na msuguano wa kugombea ardhi.

KIINI CHA MGOGORO
Mgogoro huo unadaiwa upo tangu mwaka 2008, baada ya asasi hiyo kuinunua kutoka kwa mmiliki binafsi, ambaye naye anadaiwa usahihi wa umiliki wake si bayana sana.
Ni suala lililofikia hatua ya kuwekewa kikao cha dharura na kwa mujibu wa kumbukumbu za Manispaa ya Ujiji /Kigoma, ni kwamba kilifanyika mnamo Mei 15 mwaka 2012, ambacho hakikutoa matunda mazuri ya kusuluhisha mgogoro.
Wakati kuna hatua hiyo kwa upande mmoja, katika sura ya pili nio kwamba wananchi wa kata ya Gungu walicharuka kupinga ujenzi wowote wa Kituo cha Afya kilichopo Kikungu.
Mmoja wa wazee wa mtaa wa Gungu, Bakari Mfamu, anasimulia chanzo cha mvutano huo kwamba alikuwa akiendesha kilimo cha nyanya katika sehemu hiyo, wakati eneo hilo lilipokuwa zahanati.
“Eneo hilo la hospitali halikuwa kwenye mpango wa kuendelezwa kwa wakati huo. Wanakijiji pamoja na uongozi wa hospitali ulimuacha aendelee na kilimo chake,” anaeleza Mfamu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Sultani Ndoliwa, alipoulizwa kuhusu hilo, anakiri kuwapo mkanganyiko wa sehemu hiyo ya ardhi ya kituo cha afya kuwa na wamiliki wawili, jambo linalohitaji marekebisho.
ATHARI ZA MGOGORO
Ni mgogoro uliosababisha Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji sasa unashindwa kumalizia mradi wa kujenga uzio wake na mifugo kuingia hadi jirani na wodi, jambo ambalo si sahihii.
Malalamiko mengine yaliyopo ni kwamba, kazi ya kufanya matengenezo makubwa ya Kituo cha Wilaya cha Kupambana na Kipindupindu (CTC) imekwama, kwani ni kiwanja kilichopo ndani ya eneo la mgogoro.
Sehemu ya ufafanuzi huo unatolewa na Mrisho Mtunganyoi, mjumbe wa timu ya watu sita iliyoteuliwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo.
Pia ni kati ya wazee walioeleza kwa hatua historia ya mgogoro husika, kwani wana uelewa napo kwa mapana.
Manispaa pia imejenga sehemu ya mapumziko kwa wagonjwa katika eneo hilo, lakini kwa sasa haitumiki, kutokana na walakini huo uliolezwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Manga S. Manga anasema kuwa hadi sasa kituo hicho kinahudumia takribani watu 37,400.
Anaongeza:“Hata hivyo, kimeshakosa miradi mingi ya maendeleo, ikiwamo msaada wa kujengewa chumba cha upasuaji mdogo.”
MTAZAMO WA SULUHU
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe anasema Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kigoma/ Ujiji, limepitisha uamuzi kwamba hawako tayari kumpa mtu yeyote eneo hilo, zaidi ya kudumisha huduma hizo za tiba zitolewazo na manispaa.
Kwa upande wake mwakilishi wa asasi hiyo iliyo katika mgogoro wa ardhi alipulizwa na mwandishi wa makala hii, iwapo atakubali kupewa eneo jingine kama fidia, bali malipo ya fedha. Hata hivyo hkutaja kiasi.
Katika hilo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Ndoliwa anasema mgongano wa aina hiyo, mara zote kinachoangaliwa kwanza ni maslahi ya umma na vingine vinafuata.
“Hilo ni eneo la kituo cha afya na lina maslahi ya umma. Kama kuna kosa limetendeka, linarekebishwa kwa sababu yeye yuko ndani ya Manispaa na Manispaa ndiyo ina mamlaka ya ardhi yote iliyoko ndani.
“Kama yeye anaona ana haki zaidi, tutafuata sheria na utaratibu wa kufuta kwani utaratibu uko wazi. Tena tunaweza kumshauri Waziri wa Ardhi ikaenda mpaka kwa mheshimiwa Rais, kwa sababu haiwezekani Kituo cha Afya kikamezwa kwa sababu ya maslahi ya mtu mmoja,” anatamka mkurugenzi huyo an anaongeza: “Tutakaa naye, tutaongea naye, tumshauri sababu na yeye.”
Katika hilo, Zitto, alisisitiza kuwa kilichoufikisha hapo mgogoro huo, ni mwingiliano mkubwa wa kisiasa na ufisadi wa ngazi ya chini ambao watu wengi hawauangalii.
Zitto anasema: Ili matatizo kama haya yasitokee na ili kupunguza mianya ya ufisadi, Manispaa ya Kigoma/Ujiji imejiunga katika Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Ywazi (OGP), hivyo mikataba yote sasa itaanza kuwekwa wazi kwa umma.”
Kwa mujibu wa Mkurgenzi, Mpango Mkakati wa manispaa hiyo iko katika maeneo makuu matatu, ambayo ni: Afya, elimu na kupinga rushwa.
Anasema katika mpango wa afya, kutakuwapo mfumo ambao hivi sasa unafanyiwa majaribio kuangalia mtiririko wake wa usambazaji wa dawa kuanzia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hadi kuwafikia wagonjwa.
Uongozi wa hospitali ya Gungu na wananchi wanaonufaika na huduma ya kituo hicho cha afya katika mtazamo wap wa jumla ni kwamba, serikali iangalie kwa undani mgogoro na kuusuluhisha mapema iwezekanavyo.
Ni vyema ombi hili la wananchi na uongozi wa Kituo likachukuliwa kwa uzito wake na kutekelezwa ili Kituo kipate ardhi ya kutosha kwa ajili ya miradi yake ya maendeleo itakayosaidia kituo kupata hadhi ya kuwa Kituo cha Afya kwa uhalisia badala ya jina tu kama ilivyo sasa.

Chanzo Gazeti la Nipashe
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa