Home » » Milioni 200 kupanua mfumo wa maji safi Kasulu

Milioni 200 kupanua mfumo wa maji safi Kasulu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na: Lilian Lundo – Maelezo 

Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetenga jumla ya shilingi milioni 200 katika bajeti ya Mwaka 2016/2017 ili kupanua mfumo wa maji safi katika Mji wa Kasulu.

Hayo yamesemwa leo, Bungeni Mjini Dodoma na Naibu  Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kasulu Mhe. Daniel Nswanzugwako juu ya ukabarati wa vyanzo vya maji vilivyopo Mjini Kasulu ili maji yafike katika mitaa ya kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama.

“Serikali inatambua changamoto ya mtandao wa maji inayoukabili Mji wa Kasulu, katika mwaka wa fedha 2016/17 imetenga Milioni 200 kwa ajili ya kupanua mfumo wa maji safi katika mji huo,” alisema Mhe. Kamwelwe

Aidha, Mhe. Kamwelwe aliendelea kwa kusema kuwa, fedha hizo zitatumika katika kuboresha hali ya huduma ya maji ikiwemo kuongeza mtandao wa maji Mjini Kasulu ambapo pia kata za Mrusi, Mwilavya na Kidyama zitapata huduma ya maji safi na salama.

Pia Mhe. Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zaburi kwa ajili ya mradi wa majisafi wa kujenga chujio katika Mji wa Kasulu ili kuondokana na tatizo la maji kuwa machafu.

Wizara hiyo pia imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya upanuzi wa miundombinu ya usambazaji maji Masasi – Nachingwea kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi – Nachingwea.

 Mradi huo unaohudumia wakazi wapatao 188,250 wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Halmashauri za Wilaya ya Masasi, Nachingwea na Ruangwa. Aidha wizara hiyo itaendelea kutenga fedha zaidi katika bajeti zijazo ili kupanua huduma ya upatikanaji wa maji nchi nzima.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa