Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma
RAIS John Magufuli anatarajia kuanza ziara ya siku tatu mkoani Kigoma
kuanzia kesho ambayo akiwa mkoani humo, kiongozi huyo wa nchi
anatarajia kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya ujenzi wa barabara na
miradi ya maji.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,
Emmanuel Maganga alisema Rais Magufuli atawasili kesho akitokea Kagera,
na katika siku yake ya kwanza anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nyakanazi, Biharamulo
mkoani Kagera hadi Kakonko mkoani hapa.
Maganga alisema baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Rais
Magufuli atahutubia mkutano wa hadhara Kakonko Mjini akiwa njiani kwenda
wilayani Kasulu ambako ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya
kiwango cha lami kutoka Kidahwe hadi Uvinza.
Aidha, siku ya pili ya ziara hiyo, Rais Magufuli atatembelea kukagua
maendeleo ya mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali
ya Ujerumani katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akihitimisha ziara yake ya
siku hiyo kwa kuwa na mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma.
Mkuu huyo wa mkoa alisema katika siku yake ya mwisho mkoani Kigoma,
Dk Magufuli ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji katika Mji Mdogo wa
Nguruka na kuhutubia mkutano wa hadhara, na baada ya mkutano huo
atakwenda mkoani Tabora kuendelea na ziara yake.
CHANZO HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment