Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisaini mkataba wa makubaliano mkoani Kigoma, kuhusu kushirikiana katika miradi ya maendeleo ya pamoja kati ya nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). |
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipitia mkataba wa makubaliano
katika mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa usafirishaji na uchukuzi mkoani
Kigoma,kuhusu kushirikiana katika miradi ya maendeleo ya pamoja kati ya
nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari
mkoani Kigoma, katika mkutano wa kwanza uliohusisha Mawaziri wa uchukuzi
kutoka nchi ya Tanzania, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC). Mkutano huo umejadili ushirikiano katika miradi ya
maendeleo ya pamoja baina ya nchi hizo.
…………………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesaini mkataba wa ushirikiano
katika miradi ya pamoja inayohusu masuala ya usafirishaji na uchukuzi,
lengo likiwa ni kuleta maendeleo na kukuza uchumi katika nchi wanachama.
Akizungumza mara baada ya kusaini
mkataba huo mkoani Kigoma, Waziri Mbarawa amesema kuwa mkataba huo ambao
unahusisha nchi ya Tanzania, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC), unalenga kuhuisha fursa za kiuchumi katika Ukanda wa
Ziwa Tanganyika.
Amesema pamoja na mambo mengine,
Mawaziri wa Muungano wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Nchi za Ukanda wa
Ziwa Tanganyika (LTITS), wamepokea ripoti ya wataalam inayooelekeza
utekelezaji wa miradi kwa nchi wananchama ili kufikia malengo
yanayotarajiwa.
“Tumeelekeza Sekretarieti ya
ukanda huu kuunganisha pamoja rasilimali kutoka nchi wanachama, sekta
binafsi na wadau wa maendeleo ili miradi inayotekelezwa kwa pamoja iweze
kukabiliana na changamoto za usafirishaji zilizopo katika ukanda wa
Ziwa Tanganyika”, amesema Profesa Mbarawa.
Mawaziri hao Bagiire Aggrey Henry
kutoka Uganda, Eng. Jean Bosco Ntunzwenimana kutoka Burundi na Katibu wa
Sekretarieti wa Ukanda huo Capt. Dieudonne Dukundane kwa pamoja
wamepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika
ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), na
uboreshaji wa huduma katika Mamlaka ya Bandari Tanzania ambavyo kwa
pamoja vitaunganisha Ukanda huo.
“Kukamilika kwa reli ya Kati ya
kisasa hadi Uvinza- Msongati kutawezesha reli hiyo kuunganisha vizuri
nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi na hivyo
kuchochea maendeleo katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika”, amesisitiza
Waziri wa Uchukuzi wa Burundi, Eng. Jean Bosco Ntunzwenimana.
Mawaziri hao wameelezea umuhimu wa
uboreshaji wa huduma za uchukuzi katika Bandari ya Ziwa Tanganyika ili
iwe na viwango vya kimataifa na kuunganisha vizuri ukanda huo.
Mkutano huo ni mkakati wa nchi za
Ukanda wa Ziwa Tanganyika wenye lengo la kuboresha huduma za
usafirishaji na uchukuzi katika nchi hizo ili kukuza uchumi na
kurahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment