Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma
MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema hayuko tayari
kushiriki siasa za vurugu za kupinga mipango ya Serikali ya Rais John
Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Stendi ya zamani Ujiji mjini hapa,
mbunge huyo akawashangaa baadhi ya wanasiasa nchini wanaomtaka ashiriki
vurugu za kupinga juhudi za Serikali kwa kisingizio cha kupinga Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ili kujipambanua kama wapinzani. Kabwe alisema kuwa
siasa hizo kwa sasa hazina nafasi kwake wala kwenye chama chake na
kwamba anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli na kwamba binafsi na chama
chake wamejielekeza katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kabwe alisema kuwa Mkoa wa Kigoma umekuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka
mingi hivyo kwa sasa utashirikiana na mtu yeyote mwenye mwelekeo wa
kutetea maslahi mapana ya kiuchumi bila kujali itikadi yake. Kauli ya
mbunge huyo wa jimbo la Kigoma mjini inakuja, ikiwa ni siku chache tangu
Rais John Magufuli kufanya ziara mkoani hapa na kumsifia mbunge huyo
kuwa ni kiongozi anayependa kuleta maendeleo kwa watu wake.
Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo
alikiri demokrasia kwa sasa kuwa imefinywa tofauti na huko nyuma. Kwa
upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma, Hussein Ruhava
akizugumzia halmashauri yake kupata hati chafu alikiri kuwepo kwa dosari
mbalimbali za kiutendaji na kwamba kwa sasa halmashauri yake kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kuziondoa dosari hizo.
Alisema kuwa halmashauri iko kwenye mkakati wa kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa maduka 3,000 maarufu kama Ujiji
City unaotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya China.
CHANZO HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment