Home » » SABABU WFP KUHITAJI BIL. 53/- ZA HARAKA

SABABU WFP KUHITAJI BIL. 53/- ZA HARAKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linahitaji kwa haraka jumla ya dola za Marekani milioni 23.6 (sawa na Sh. bilioni 52.8) kuanzia sasa hadi Desemba ili kumudu kuendelea kutoa mgao unaokidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi wanaoishi nchini.

WFP limelazimika kupunguza mgao wa chakula kinachotolewa kwa wakimbizi 320,000 wanaoishi katika kambi za Mtendeli, Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma kwasababu ya upungufu wa fedha.
Shirika la WFP hugawa vyakula vya aina tano tofauti kwa wakimbizi, wengi wao wakiwa wanatoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC). Vyakula hivyo ni unga wa mahindi, kunde, nafaka kuu, mafuta ya mbogamboga na chumvi. 

Kwa sababu ya upungufu wa fedha, aina zote tano za vyakula kwa mwezi huu zinakidhi tu asilimia 62 ya kiasi cha kalori 2,100 zinazopendekezwa kitaalamu kutosha mahitaji ya mtu ya siku.

“Pasipo mwitikio wa haraka kutoka kwa wahisani, itakuwa lazima kupunguza mgao kwani akiba ya chakula inapungua kwa kasi sana,” alisema Mwakilishi wa Nchi wa WFP Tanzania, Michael Dunford.
“Wakati ambapo WFP inashukuru sana kwa msaada uliokwishatolewa hadi sasa, tunatoa wito ili wahisani waitikie haraka na kuwasaidia wakimbizi na kutoa fedha zaidi ili tugawe mgao kamili na kuzuia athari mbaya zisidumu kwa muda mrefu.” 

Kupunguza mgao kunasababisha matatizo mengi yanayoweza kubadili vibaya maisha ya wakimbizi. Kupunguza kiasi cha kalori na msaada wa lishe kunaweza kusababisha utapiamlo mkali na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa, imeelezwa. 

Licha ya aina hizo tano za vyakula, WFP pia hugawa vyakula vya moto kwa wakimbizi mara baada ya kuwasili, mgao wa chakula cha nyongeza kwa wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha na msaada wa chakula kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini na kwa watu wanaoishi na VVU.
Hadi sasa vyakula vya moto vinavyogawiwa kwa wakimbizi wanaoingia nchini na programu ya chakula cha nyongeza havija athiriwa na punguzo la sasa la mgao.

WFP NI NINI?
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) ndiyo wakala ya kiutu kubwa zaidi linalopambana na njaa kote ulimwenguni, huku likitoa msaada wa chakula katika nyakati za dharura na kushirikiana na jamii ili kuimarisha lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru. Kilamwaka, WFP linatoa msaada kwa watu wapatao milioni 80 katika nchi 80.


Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa