Imeandikwa na Waandishi Wetu
WATU watano wameuawa katika matukio mawili ya ujambazi kwenye mikoa ya Kigoma na Katavi.
Taarifa za Kipolisi zinasema kwamba majambazi wanne waliuawa na watu
watatu wakijeruhi wakati wa majibizano kati ya Polisi mkoani Katavi na
majambazi katika Kijiji cha cha Kahenze, Kata ya Ugala wilayani Mpanda.
Majibizano hayo yalichukua robo saa. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa,
Benedict Mapujila alisema marehemu hao walikutwa na silaha mbili za
vita aina ya SMG zenye namba za usajili UA 5538, 1997 na AFV 0826, 1996
zikiwa na jumla ya risasi 27 katika magazine zake.
Kaimu Kamanda Mapujila amesema kwamba majina ya marehemu
yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi. Imeelezwa na Mapujila kuwa siku
moja kabla ya kuuawa kwao watu hao wanne walimpora mfanyabiashara,
Shija Masanja pesa taslimu shilingi laki nane na simu mbili aina ya
Tecno.
Nako Mkoani Kigoma, mtu mmoja amekufa na wengine watatu wamejeruhiwa
katika tukio la ujambazi kutokana na gari walilokuwa wakisafiria
kushambuliwa kwa risasi ikiwa ni jaribio la kuliteka gari hilo. Tukio
hilo lilitokea jana katika Kijiji cha Narulanga Wilaya ya Kibondo,
ambako gari dogo la abiria (maarufu kama mchomoko) lenye namba za
usajiri T415 DHM lililokuwa linaendeshwa na dereva Miraj Seif (28)
lilishambuliwa wakati likitoka Kasulu kwenda Kibondo.
Mkuu wa Wilaya Kibondo, Luis Bura alithibitisha kutokea kwa shambulio
hilo na kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vimeanza msako wa
kuwatafuta majambazi hao huku hatua za kudhibiti vitendo vya ujambazi
zikiendelea kuimarishwa.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Kizito Luamvya
alisema alipokea watu wanne waliokuwa na majeraha kwenye miili yao na
kwamba mmoja alifariki dunia hospitalini hapo akiwa anapatiwa matibabu.
Alimtaja aliyefariki kuwa ni Regna Petro (14) ambaye ni mwanafunzi
Shule ya Msingi Nyarulanga, kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya
kupata majeraha makubwa ya risasi tumboni. Aliwataja majeruhi wa tukio
hilo kuwa ni Grace Malulu (11) mwanafunzi wa darasa la pili, Stanford
Chubwa (48) ambaye alijeruhiwa vibaya usoni baada ya risasi kutoboa
jicho lake moja na Edna Johachim aliyepatiwa matibabu na kuruhusiwa
kurudi nyumbani.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment