Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma
WANAFUNZI wa shule za msingi na sekondari mkoani Kigoma, wametakiwa
kutumia maktaba kusoma vitabu na machapisho mbalimbali kwenye maktaba
hizo, kuongeza ufahamu na uelewa wa mambo mbalimbali yanayohusiana na
masomo yao.
Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava ametoa kauli hiyo
katika kongamano la kushindanisha wanafunzi kusoma, lililoandaliwa na
Shirika lisilo la kiserikali la Kigoma Women Development Group (KIWODE).
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Diwani wa Kata ya
Kasingirima, Nassoro Hamduni alisema kwa wanafunzi kutumia muda wao wa
ziada kusoma vitabu na machapisho mbalimbali yanayohusu masomo yao baada
ya muda wa mafunzo darasani, kuna nafasi kubwa ya kuwawezesha wanafunzi
kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Akisoma risala ya kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kiwode, Sophia
Patrick alisema pamoja na kuongeza ari ya wanafunzi kupenda na kuongeza
uwezo wao wa kusoma, pia kongamano hilo linatumika kuwaweka pamoja wadau
wa elimu kujadili changamoto zinazowakabili na hatua za kuchukua
kulingana na nafasi zao na rasilimali zinazowazunguka.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment