ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila
amejivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amefanya hivyo kwa kile alichodai kuwa hana imani tena na upinzani, kama
jukwaa salama la kupambana na ufisadi.
Kafulila amesema kuwa vyama vya upinzani nchini vimepigwa ganzi na
kupooza ghafla katika harakati zake za kupambana na ufisadi, baada ya
Rais Dk John Magufuli kuendesha vita hiyo kwa mafanikio makubwa.
Alisema mafanikio hayo ya Rais Magufuli, yameufanya upinzani kuwa
siyo jukwaa salama tena katika vita dhidi ya ufisadi; na ndiyo maana kwa
hiari na utashi wake, ameamua kujivua uanachama wa Chadema.
“Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, vita ya miaka mingi dhidi ya
ufisadi imechukua sura mpya. Watuhumiwa na wahusika wa rushwa kubwakubwa
ambao walikuwa hawaguswi, tunashuhudia wakifikishwa mbele ya vyombo vya
sheria, juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono na watu wote na vyama vyote
vilivyojipambanua kupambana na ufisadi,” alieleza Kafulila.
Kwa mujibu wa Kafulila, ambaye siku zote alijipambanua na kujitoa
muhanga kupambana na ufisadi kupitia jukwaa la Bunge, vyama vya siasa na
shughuli za kijamii kwa ujumla, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,
vyama vya upinzani nchini vinaonekana kupigwa ganzi na kupooza katika
juhudi zake za kupambana na ufisadi.
Baada ya kujivua uanachama, Kafulila alisema kuwa atatangaza siku za
hivi karibuni jukwaa jipya la harakati zake dhidi ya ufisadi. Maamuzi
hayo ya Kafulila yanakuja siku moja tu baada ya wanasiasa sita kutoka
vyama vya upinzani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Wanasiasa hao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof.
Kitila Mkumbo (ACT-Wazalendo), Lawrence Masha (Chadema), Patrobas
Katambi (Chadema), Edna Sunga (ACT-Wazalendo), Samson Mwigamba
(ACTWazalendo) na Albert Msando (ACT-Wazalendo).
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema jana
kuwa kuna wanasiasa zaidi ya 200, wameomba kujiunga na chama hicho
tawala. Ikumbukwe kuwa mwaka jana Kafulila alihama NCCR-Mageuzi na
kujiunga Chadema, akieleza kuwa alikwenda huko kwa kuwa ni muhimu kwa
watu wenye nia ya mabadiliko kuwa katika chama kimoja ili kufupisha
safari.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema kuwa anamtakia
kila heri Kafulila, lakini akaeleza kuwa Kafulila si mkaaji kokote
anakoenda. Dk Mashinji alisema, “Kama Chadema tunamtakia kila la heri,
sisi hatuna shida na yeye kuhama kwa sababu amekuwa akihama kila siku.
Alianza Chadema, akaenda NCCR -Mageuzi, kisha akarudi Chadema. Sasa
sijui anaenda CCM lakini si mkaaji.” Imeandaliwa na Matern Kayera na
Regina Mpogolo
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment