Home » » KUJIRUDIA KWA MAKOSA YA KISWAHILI

KUJIRUDIA KWA MAKOSA YA KISWAHILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  
Katika mfululizo wa makala zangu, nimejikita zaidi katika kuyachambua magazeti ya Kiswahili kwa lengo la upunguza makosa yanayojitokeza ama ya kisarufi au ya kifasihi.
Kwa bahati mbaya wanaosoma makala zangu na kuleta mrejesho ni wasomaji wachache tena ni wa kawaida tu. Hajatokea mwandishi wa magazeti au hata mhariri anayejali kusoma kwa makini ili kutoa maoni yake kwa lengo la kuyarekebisha.
Makosa mengi yanajirudia, hata baada ya kuyatolea ufafanuzi ikiwa ni dalili tosha kuwa waandishi hawasomi na kama wanasoma hawabadiliki.
Matokeo haya, hayanikatishi tamaa nami nitaendelea na kazi yangu hii.
Mapema mwezi uliopita iliandikwa,
” Shirika hilo lilisema kuwa la kusikitisha zaidi ni kwamba baadhi ya wavuvi walioathirika ni wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.”
Yako maneno mawili yanayotatanisha, nayo ni wahanga na waathirika. Mhanga ni utoaji wa kafara. Kujitoa mhanga ni kitendo kinachoweza kuhatarisha maisha kwa ajili ya upigania masilahi yako au ya mtu mwingine. Athiri ni kutia doa au dosari , jeruhi na kadhalika.
Kwa hiyo, nomino inayoweza kupatikana kutokana na kulinyambua neno athiri ni muathiriwa kwa maana ya mtu aliyejeruhiwa au aliyepata doa au dosari kutokana na kitendo fulani.
Kwa hiyo, siyo sahihi kuwaita walioathirika kuwa ni wahanga.
“ San Kroenke amesaini mkataba wa kuinoa timu hiyo.”
Neno saini limetolewa kutoka katika lugha ya Kiingereza . Kwa Kiingereza neno hili hutumika kama nomino au kitenzi. Waswahili walipolikopa neno hili, walipenda kulitumia kama nomino tu na hadi sasa haya ndiyo matumizi yaliyoenea. Kulitumia vinginevyo, tunavunja utaratibu uliokubaliwa na wengi.
Badala ya kusaini mkataba, pangetumiwa kutia saini au kuweka saini mkataba.
Kiusahihi ingesomeka, “San Kroenke ametia saini /ameweka saini mkataba mpya wa kuinoa timu hiyo.”
Msomaji mmoja aliwahi kuandika kuwa neno changamoto linatumika vibaya pamoja na kwamba kisawe chake ni ‘challenge’ kwa lugha ya Kiingereza. Mwandishi aliandika,
“ Wazee wa wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera watanufaika na ushauri wa kisheria hivyo, kuondokana na changamoto zinazowakabili katika maisha.”
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), neno changamoto lina maana ya hamasa, kutia ari, kuwa na hamu ya kufanya jambo. Lilipobadilishwa maana na kuanza kutumiwa tofauti na maana asilia, linawakanganya wasomaji wengi. Badala ya kutumia changamoto, yangetolewa maelezo kama ‘baadhi ya matatizo yanayowakabili.’
Ifahamike kuwa lugha ya mazungumzo ni tofauti kwa kiasi fulani na lugha ya maandishi. Kwa mfano neno ‘natumai’ linatumika katika mazungumzo, ila katika uandishi ni sahihi kuandika ‘natumaini’. Kwa mfano iliandikwa,“ Mwendesha Mashtaka Gerrie Nel alisema kuwa alitumai kumaliza kumhoji mwana riadha huyo siku ya Jumanne.”
Pamoja na kuandika neno natumai badala ya natumaini, maneno ‘siku ya Jumanne’ limeandikwa bila sababu ya msingi. Jumanne ni siku, hivyo haipo haja ya kuongeza neno ‘siku’ ambalo siyo lazima liandikwe. Kwa usahihi ingeandikwa,“ Mwendesha mashtaka Gerrie Nel alisema kuwa alitumaini kumaliza kumhoji mwanariadha huyo Jumanne.”
“ Hakika nimehemewa kiasi kwamba nakosa maneno mazuri ya kuelezea furaha yangu na shukurani zangu kwenu kwa heshima kubwa mliyonipa.”
Matumizi ya neno ‘hemewa” limetumika isivyo. Kuhemewa maana yake ni kuzongwa na kazi nyingi, kuchoka kutokana na kazi nyingi.
Mhusika alitaka kusema kuwa alizidiwa au alizongwa na mawazo mengi kiasi kwamba alishingwa kupata maneno ya kutoa shukrani kwa heshima aliyopewa.
0716 694240
Chanzo;MwananchI

1 comments:

Unknown said...

Asante sana. Namijifunza maneno machache kupitia habari hii

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa