Home » » 20 WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI KIGOMA

20 WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI KIGOMA


Na Emma J Matinde
KIGOMA
Wednesday June 28, 2012
Watu 20 wamejeruhiwa baada ya basi walililokuwa wakisafiria kutoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam kupata ajali jana asubuhi katika eneo la Gungu manispaa ya Kigoma Ujiji
Ajali hiyo imetokea majira ya saa kumi na mbili asubuhi katika barabara ya Kigoma-Kasulu na kulihusisha basi la abiria lenye namba T369 ASE aina ya Scania mali ya kampuni ya KIMOTCO lililokuwa likiendeshwa na dereva Mohamed Bakari mkazi wa Dar es Salaam ambapo liliacha njia na kutumbukia mtaroni
Majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika hospitali ya mkoa ya Maweni kwa ajili ya matibabu ambapo Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dr. Leonard Subi amethibitisha kupokea majeruhi hao 17 wakiwa ni wanaume na 3 wanawake.
Amesema kati ya waliojeruhiwa 17 wametibiwa na kuruhusiwa huku wengine 3 wakilazwa kwa ajili ya kuendelea kuchunguzwa afya zao ambapo mmoja miongoni mwao ni mwanamke.
Akisimulia ajali hiyo mmoja wa majeruhi hao Bi.Stumay Mushi mkazi wa Ujiji Kigoma ambaye alikuwa anasafiri kuelekea Dar es Salaam amesema kabla ya kuanza safari dereva wa basi hilo bw.Mohamed Bakari mndengereko mkazi wa Dar es Salaam alisimama na kujitambulisha kwa abiria na kuwataka abiri wote kutanguliza mbele ya safari yao
“kabla ya kuondoka dereva akasimama akajitambulisha kwamba jamani wasafiri mlioko ndani ya basi hili, najitambulisha mimi ni dereva wenu naitwa Mohamed Bakari Kipanga kwa hiyo naomba dua zetu ziwe moja tuweze kufika safari yetu kwa salama na ntakapokwenda tofauti na sheria mnieleze, kama ntakuwa na mwendo mkali mnieleze ili tuweze kufika salama”,alisema abiria huyo.
Jeshi la polisi mkoani Kigoma limethibitisha kutokea kwa ajali na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni uzembe ambapo dereva wa basi hilo bw.Mohamed Bakari anashikiliwa na polisi kwa kuendesha gari kwa uzembe.
Awali basi hilo ambalo lilikuwa limefika Kigoma kwa mara ya kwanza lilikuwa limekodiwa kupeleka vijana wanaokwenda kujiunga na mafunzo ya JKT katika kambi ya JKT Bulombora mkoani Kigoma na baadaye kuomba kibali cha kusafirisha abiria waendao Dar es Salaam na ndipo wakakutwa balaa hilo
EndS

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa