na Mwemezi Muhingo, Kibondo
KIKAO cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kilichofanyika jana kimeridhia kwa kauli moja kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simon Kanguye.
Taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Leopord Ulaya ilisema kuwa alipokea barua ya kujiuzulu kwa mwenyekiti huyo Juni 22 jioni.
Alisema Kanguye aliamua kujiuzulu wadhifa wake baada ya madiwani 27 wa halmashauri hiyo kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye ndipo akaamua kuachia ngazi ili kulinda heshima ya halmashauri.
Alisema kuwa kikao hicho cha kiliandaliwa kwa kwa ajili ya kumtoa madarakani kwa nguvu mwenyekiti endapo asingejiuzulu mwenyewe baada ya kupigiwa kura hizo.
Alieleza kwamba kwa upande wake Kanguye alisema kuwa yeye ameamua kujiuzulu mwenyewe bila shinikizo la mtu yeyote ili kulinda heshima yake na halmashauri yake na baada ya kuona vurugu zinaanza kutokea kwa madiwani anao waongoza.
Awali Kanguye alikuwa akishututumiwa na baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kwa kushindwa kuiongoza Halmashauri hiyo badala yake kujilimbikizia mali tofauti na kipato anachopata jambo ambalo mwenyewe alilipinga na kudai kuwa hayo ni maneno ya kisiasa yanayotaka kumchafua.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Venance Mwamoto kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alisema kitendo cha Kanguye kuamua kuachia madaraka ni cha kiungwana na ni demokrasia hasa panapotokea tatizo la kiutendaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa sasa itaongozwa kwa muda na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juma Maganga, kama Mwenyekiti mpaka pale uchaguzi wa nafasi hiyo utakapofanyika baada ya siku 60 kuanzia hivi sasa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment