Home » » Serukamba amsifu Mwakyembe kupanda Treni

Serukamba amsifu Mwakyembe kupanda Treni



Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu

MBUNGE wa Kigoma Mjini (C.C.M) Peter Serukamba amesifu hatua ya Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ya kutumia usafiri wa reli kwenda mjini Dodoma kwa kuwa hatua hiyo inaonyesha nia yake ya dhati ya kulifufua Shirika la Reli Tanzania (TRL).

Akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM asubuhi ya leo Serukamba amesema kuwa kitendo cha waziri huyo kutumia usafiri huo wa reli kutamfanya ayajue matatizo ya reli ambayo wabunge wamekuwa wakipigia kelele bungeni na kupuuzwa.

Alisema kutengemaa kwa reli ya kati na nyingine sio tu kutachochea maendeleo ya taifa bali pia kitaongeza uzalishaji wa wananchi na kupunguza ukali wa maisha ambao kwa sasa umekuwa ni wimbo wa taifa katika kila kona ya nchi.
Serukamba ambaye yuko mjini Dodoma Bungeni alisema “Hatua ya Dk Mwakyembe itamsaidia kujionea hali halisi ya kile ambacho tumekuwa tukikilalamikia kila siku, maana hawa viongozi wetu wa juu mara nyingi hufanya kazi ofisini tu bila kujionea hali halisi ya mambo”.

Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe jana alitumia usafiri wa treni kwenda bungeni mjini Dodoma jambo ambalo limegusa hisia za watu wengi na wengi wao wakiweka matumaini makubwa juu ya utendaji wa waziri huyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa