Home » » WAKULIMA WA MIHOGO WALALAMIKIA SOKO LA UHAKIKA

WAKULIMA WA MIHOGO WALALAMIKIA SOKO LA UHAKIKA

Na Iddi Risasi, Kigoma

WAKULIMA wa migomba na mihogo mkoani Kigoma wamelalamikia kutokuwapo kwa masoko ya uhakika kwa ajili ya uuzaji wa mazao yao, jambo linalowakatisha tamaa ya kuongeza uzalishaji.

Wakizungumza na MTANZANIA mjini hapa, wakulima kutoka maeno mbalimbali ya Kigoma wamesema kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji katika mazao hayo, lakini kwa sasa wanakumbana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa masoko.

Claudio Marco, ambaye ni mkulima wa mihogo kutoka Kijiji cha Nyachenda, wilayani Kasulu, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji kwa wakulima katika zao hilo na hiyo inatokana na upatikanaji wa mbegu bora na zinazohimili magonjwa.

Alisema baada ya uzalishaji kuongezeka maradufu wamekuwa na tabu ya masoko na hivyo kutegemea soko moja la Burundi ambalo bei zake zinalingana na faida kidogo kulingana na gharama za uzalishaji.

Naye, Ernest Ndabalinza, mkulima wa ndizi kutoka Kijiji cha Kibwigwa mpakani na Burundi wilayani Kasulu, alisema kwa sasa wakulima katika Tarafa ya Manyovu wameongeza uzalishaji na kulima ndizi kubwa zenye urefu.

Alisema mkungu wenye urefu wa futi saba umekuwa hauna bei na kuuza kwa kati ya Sh 5,000 na Sh 7,000, jambo ambalo kwao ni hasara kulingana na gharama za uzalishaji.

Waliiomba Serikali pamoja na mipango mbalimbali ya kuongeza uzalishaji, lakini pia haina budi kuwawekea miundombinu na fursa za kutosha za kuwawezesha kupata masoko ya uhakika kwa ajili ya mazao yao.

Akizungumzia malalamiko hayo, Ofisa Kilimo na Mifugo Wilaya ya Kasulu, Manoni Odillo, alisema tayari tatizo hilo limeshaanza kufanyiwa kazi, ikiwamo kuimarisha barabara za kuingia na kutoka mashambani lakini pia kuimarisha barabara kwenda nje ya mkoa na nje ya nchi.

Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji kutokana na wakulima kuzingatia kanuni za uzalishaji bora wa mazao unaotokana na mafundisho wanayopata katika mashamba darasa na kuwatumia wakulima wawezeshaji katika kuwasaidia wakulima wenzao.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa