Baadhi ya vifaa na miti shamba kwa ajili ya kufanyia matibabu kwa watu wenye ugonjwa wa bengu.
Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu
Wakazi wa mkoa wa Kigoma, wanakabiliwa na changamoto ya maradhi ya Bengu (dondatumbo) ambayo huwakumba watoto wadogo hasa walio chini ya miaka mitano mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na wakazi wa Mkoa huo kufuatia vifo vya watoto vinavyosababishwa na Ugonjwa huo
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakazi wa Mkoa huo na madactari walisema kuwa ugojwa huo wa Bengu unafahamika chanzo chake,tiba pamoja na kinga,ambapo wakazi wake walikiri kufahamu maradhi hayo na hutumia tiba asilia kutibu ugonjwa huo.
Walisema kuwa Ugonjwa wa Bengu (donda tumbo) umekuwa na tabia ya kuwashambulia watoto wadogo ambapo dalili zake hurandana na mtoto aliye na ugonjwa wa utapiamlo,ambapo kwa wageni wa mkoa huo hupata shida kutambua dalili hizo.
Tabibu anayetibu kwa kutumia dawa asilia Anzelami Byongo alisema Ugonjwa wa bengu umeanza kujitokeza Miaka ya 1980,baada ya maingiliano baina ya raia toka Burundi ,Rwanda na Congo,huku akikiri kurithi tiba hizo toka enzi za wazee wao ambao nao walioteshwa Manamba.
“dalili zake hazitofautiani na mtoto mwenye ugonjwa wa utapiamlo kwani nywele hubadilika na kuwa rangi ya kahawia, ngozi yake hujikunja na kupauka kama majivu,hutokwa na vipele vidogovidogo pamoja na kuharisha kinyesi cha majimaji ambayo yanamafuta “ amesema Byongo.
Byongo alibainisha kuwa pamoja na dalili hizo pia mtoto huanza kuharisha na kutapika pindi alapo chakula na kadiri anavyougua fupa la uti wa mgongo hujitokeza hali inayotishia kupoteza uhai wa mtoto.
Katika kujua chanzo cha maradhi haya Byongo amesema hajajua chanzo kamili ingawa husadikika umetokea DRC ,japo tiba za hospitali hazina uwezo wa kutatua changamoto hiyo,kwani wengi hurudia dawa za miti ya asili ambazo huchanganywa na za hospitali .
Akizitaja baadhi ya tiba za ugonjwa wa Bengu Byongo alisema ni mtunza Makaburi,Tetesaclini ,Majani ya mwembe, Peremende (dawa ya mende) ambayo huchanganywa na maji kwa kufuata kiwango maalum cha umri wa mtoto na kutiwa kwenye mpira maalum na kumwinama maji hayo yenye mchanganyiko wa dawa( kupitia njia ya haja kubwa) ambapo kiasili huitwa ( Mwino).
Kwa upande wake Diwani wa viti maalum kata ya Mwamgongo Hidaya Kwapi alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na tiba zake ni miti ya asili na alishindwa kubainisha chanzo cha ugonjwa huo,japo alikiri maradhi hayo hutoka nchi za jirani hali inayowafanya wakazi wengi wa Mkoa wa kigoma kuwa na Mwino (mabomba) ili kujipatia huduma hiyo inapolazimu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kigoma vijijini John Kilimba alipoulizwa ugonjwa wa bengu kwa watoto wadogo alishindwa kulitolea ufafanuzi kamili, kwa kusema kuwa, hajawahi kumuona mtoto mwenye shida hiyo pia hajawahi kuusikia ugojwa huo.
Dr.Kilimba alisema kuna uwezekano wa ugojwa huo kuwepo lakini jamii husika ikaishia kwenye tiba asilia pasipo wao kujua na kudai kuwa labda hospitali ya mkoa wanaweza wakalijua hilo.
Ugonjwa wa bengu ( donda tumbo) umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo kwa miaka nenda rudi mkoani humo hali inayotishia hata ukuaji bora wa mtoto pindi achelewapo kupata tiba kwa wakati.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment